Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vita ya kibabe Championship!

CHAMPIONSHIP Pict

Muktasari:

  • Songea United inayoburuza mkia katika nafasi ya 15 ikiwa na pointi sita, itakuwa na kibarua kigumu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, itakapokabiliana na Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 18.

LIGI ya Championship imeingia raundi ya 10, huku jana Ijumaa mechi mbili zikichezwa katika viwanja mbalimbali, nyingine tatu zikipigwa leo Jumamosi na raundi hiyo kuhitimishwa kesho Jumapili. Ushindani unazidi kushika kasi kutokana na kila timu kuhitaji matokeo mazuri ili kuboresha nafasi yake kwenye msimamo.

Katika mechi za jana Ijumaa, Gunners FC, iliyoichapa Tabora United bao 1-0, ilikuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma, kucheza na IAA ya Arusha, iliyokuwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons.

Nayo Transit Camp, iliyotoka kuchapwa mabao 3-2 na Mbuni ya Arusha katika mchezo uliopita, ilikuwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar kuikabili Tabora United, iliyokuwa imetoka kupoteza mbele ya Gunners.

CHAMP 04

Leo Jumamosi zitapigwa mechi tatu, ambapo kwenye Uwanja wa Aga Khan, Arusha, Mbuni itakuwa mwenyeji wa Stand United ‘Chama la Wana’, inayotaka kurejea kwenye ushindi baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na KenGold katika mchezo uliopita.

Mbuni inashika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 11, huku Stand United ikiwa ya sita na pointi 14. Mbuni itategemea zaidi mchango wa washambuliaji wake Ezekiel Zonobi na Mussa Mpina, ambao wameifungia timu hiyo mabao manne kila mmoja.

Kwa upande wa Stand United, Raymond Masota na Lee Oraph Komba ni miongoni mwa wachezaji wanaotegemewa katika safu ya ushambuliaji, kila mmoja akiwa amefunga mabao mawili.

CHAMP 07

Songea United inayoburuza mkia katika nafasi ya 15 ikiwa na pointi sita, itakuwa na kibarua kigumu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, itakapokabiliana na Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 18.

Songea inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Bigman FC ya jijini Tanga. Hata hivyo, changamoto kubwa inayokikabili kikosi hicho ni udhaifu wa safu zake za ushambuliaji na ulinzi, baada ya kufunga mabao manne pekee na kuruhusu 11 katika mechi tisa ilizocheza.

Kwa upande wa Mtibwa Sugar, inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali baada ya kuichapa TMA ya Iringa bao 1-0 ugenini wiki iliyopita. Timu hiyo imeonesha uimara zaidi ikilinganishwa na wapinzani wake, ikiwa imefunga mabao 10 na kuruhusu sita katika mechi tisa.

CHAMP 01

Mechi nyingine ya leo itachezwa kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Chunya, jijini Mbeya, ambapo wenyeji KenGold  wataikaribisha TMA ya Iringa. KenGold inaingia kwenye mchezo huo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Stand United, huku TMA ikihitaji ushindi ili kujinasua kutoka nafasi ya mwisho ya msimamo.

KenGold inashika nafasi ya 13 ikiwa na pointi tisa, baada ya kushinda mechi mbili, kutoka sare tatu na kupoteza nne. Kwa upande wa TMA, inashika nafasi ya 16 ikiwa na pointi mbili, baada ya kushinda mchezo mmoja, kutoka sare mbili na kupoteza sita.

Raundi ya 10 itahitimishwa kesho Jumapili kwa mechi tatu, ambapo Bandari Tanzania itakuwa mwenyeji wa maafande wa Rhino Rangers kutoka mjini Tabora kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

CHAMP 04

Bandari inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kuichapa Kigamboni United bao 1-0 katika mechi iliyopita. Timu hiyo inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 17, huku Rhino Rangers ikiwa ya tano kwa pointi 15, jambo linalofanya mchezo huo kuwa muhimu kwa timu zote katika harakati za kujiimarisha kwenye nafasi za juu.

Rhino Rangers, iliyoshinda mechi nne, kutoka sare tatu na kupoteza mbili kati ya tisa ilizocheza, inahitaji matokeo mazuri ili kuendelea kuisogelea Bandari. Katika mchezo uliopita, ililazimishwa sare ya bao 1-1 na KMC.

Katika mchezo mwingine wa kesho, Kigamboni United itakuwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, kuikaribisha Bigman ya jijini Tanga. Kigamboni inaingia kwenye mchezo huo baada ya kupoteza dhidi ya Bandari Tanzania, huku Bigman ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuichapa Songea United mabao 2-0.

CHAMP 01

Kigamboni United inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi 12, baada ya kushinda mechi tatu, kutoka sare tatu na kupoteza tatu. Kwa upande wa Bigman, inashika nafasi ya 12 ikiwa na pointi 10, hivyo mchezo huo ni muhimu kwa timu zote katika jitihada za kupanda kwenye msimamo.

Mechi ya mwisho kesho Jumapili itapigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, ambapo Tanzania Prisons itakuwa mwenyeji wa vinara wa ligi hiyo, KMC.

Prisons inaingia kwenye mchezo huo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya IAA ya Arusha, huku KMC nayo ikitoka sare kama hiyo dhidi ya Rhino Rangers.

KMC inaongoza ligi ikiwa na pointi 19, huku Prisons ikiwa nafasi ya tatu na pointi 17, hivyo mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na nafasi za timu hizo kwenye msimamo. Prisons itamtegemea mshambuliaji wake nyota, Oscar Paul, aliyewahi kuichezea KMC msimu uliopita. Hadi sasa ameifungia Prisons mabao sita kati ya 14 iliyofunga msimu huu, akiwa kinara wa ufungaji ndani ya kikosi hicho.

CHAMP 02

Kwa upande wa KMC, itamtegemea mshambuliaji wake Ramadhan Hashim Kalanje, ambaye ameifungia timu hiyo mabao tisa kati ya 17 iliyofunga. Kwa idadi hiyo anashika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji wa ligi nyuma ya Hamdan Sarhani wa Transit Camp, aliyefunga mabao 11.

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, alisema anatarajia mchezo mgumu kutokana na ubora wa kikosi cha KMC msimu huu, hasa ikizingatiwa kuwa timu hiyo haijapoteza mchezo wowote hadi sasa. Hata hivyo, alisema wamejipanga vizuri kukabiliana na wapinzani wao.

Kocha Mkuu wa KMC, Mohamed Muya alisema amewasisitizia wachezaji wake kucheza kwa nidhamu, kujilinda vizuri na kutowapa wapinzani nafasi ya kutengeneza mashambulizi mengi.