Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kagame 2024 mwisho wa ubishi, ni APR au Red Arrows!

Muktasari:

  • Timu hizo zimefuzu hatua hiyo baada ya kushinda mechi za nusu fainali, APR ikiizima Al Hilal ya Sudan kwa penalti 5-4 baada ya dakika 120 kumalizika bila ya bao lolote, huku Wazambia wakitumia dakika 30 za nyongeza kuwafumua Al Wadi pia ya Sudan kwa mabao 2-0.

FAINALI za 47 za Klabu Bingwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame 2024 zitafikia tamati kesho Jumapili. Fainali hiyo inayopigwa kuanzia saa 9:00 alasiri inazikutanisha APR ya Rwanda inayosaka taji la nne la michuano hiyo dhidi ya waalikwa kutoka Zambia, Red Arrows.

Timu hizo zimefuzu hatua hiyo baada ya kushinda mechi za nusu fainali, APR ikiizima Al Hilal ya Sudan kwa penalti 5-4 baada ya dakika 120 kumalizika bila ya bao lolote, huku Wazambia wakitumia dakika 30 za nyongeza kuwafumua Al Wadi pia ya Sudan kwa mabao 2-0.

Hii itakuwa ni fainali za tisa kwa Wanyarwanda, inayosaka taji la nne la michuano hiyo iliyopewa jina la Kagame Cup kuanzia mwaka 2002 baada ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame kujitosa kuidhamini.

APR ilishacheza awali fainali nane tofauti tatu ikifanikiwa kutwaa ubingwa 2004, 2007 na 2010, huku ikipoteza nyingine tano za 1996, 2000, 2005, 2023 na 2014. Kwa Maafande wa Red Arrows kutoka Zambia walioshiriki kama timu mwalikwa, hizo ni fainali za kwanza za Kagame, na ilipenya nusu fainali ikiwa mshindwa bora (best looser) kutoka Kundi B. Red Arrows ilimaliza nafasi ya pili kwa kuvuna pointi sita katika mechi tatu nyuma ya vinara Al Hilal iliyomaliza na pointi tisa ikiwa timu pekee iliyoshinda mechi zote tatu za makundi ya michuano hiyo iliyoanza Julai 9 ikishirikisha timu 12 na kuchezwa kwenye viwanja vya KMC uliopo Mwenge na Azam Complex, Chamazi vyote vya jijini Dar es Salaam.

Timu hiyo ni ya kwanza kutoka Zambia kufika fainali za michuano ya Kagame, lakini inakuwa ni ya nne kutoka Ukanda wa Soka wa Kusini mwa Afrika (Cosafa) baada ya Rio Tinto ya Zimbabwe iliyocherzwa fainali za mwaka 1982 na kupoteza mbele ya AFC Leopards ya Kenya.

Klabu ya pili kucheza fainali hizo ilikuwa ni ADMARC Tigers ya Malawi iliyopoteza 2-1 kwa AFC Leopards mwaka 1983 na Big Bullets pia ya Malawi ilikuwa timu ya mwisho kucheza hatua hiyo mwaka 2021 na kulala bao 1-0 mbele ya Express ya Uganda.

Kama itaendelea kucheza soka ililoonyesha tangu mwanzo wa michuano mwaka huu kisha kubeba ubingwa, itakuwa ni timu ya kwanza ya Cosafa kutwaa ubingwa wa Kagame, kwani tangu michuano ilipoasisiwa 1967 haijawahi kutokea.


MZUKA KIDOGO, ILA FRESHI

Licha ya kukosekana klabu wenyeji na wazoefu wa michuano hiyo, Simba, Yanga na Azam kumeifanya Kagame Cup 2024 kutokuwa na msisimko mkubwa, lakini boli limepigwa na mashabiki waliohudhuria mechi kuanzia zile za makundi hadi nusu fainali wamepata burudani.

Licha ya wenyeji Singida Black Stars, Coastal Union na JKU kushindwa kufurukuta na kutolewa hatua ya makundi, bado mashabiki waliendelea kuifuatilia michuano hiyo kutokana na kuvutiwa na soka lililopigwa.

Timu zote nne zilizokuwa zimetinga nusu fainali zilionyesha soka tamu kwelikweli na la ushindani, huku Wasudan wakitawala kwa kiasi kikubwa, licha ya kwanza timu zao zote zimetolewa kwenye hatua hiyo kwa maana ya Al Wadi na Al Hilal. Katika mechi za makundi timu hizo hazikupoteza kama ilivyokuwa kwa APR, huku Red Arrows ikipoteza moja.

Al Wadi ilianza michuano kwa kuinyoa JKU ya Zanzibar kwa bao 1-0, kisha kuifunga Dekadaha ya Somalia kwa mabao 2-1 na kumalizia na sare ya 1-1 na Wagosi wa Kaya, Coastal Union iliyowahi kufika fainali za michuano hiyo mwaka 1989 na kupoteza mbele ya Kenya Breweries (sasa Tusker Kenya) kwa mabao 3-0. Wababe hao walimaliza kama vinara wa Kundi A kwa kukusanya pointi saba na kupangwa kukutana na Red Arrows iliyoshika nafasi ya pili katika Kundi B ikianza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, kabla ya kufumuliwa mabao 5-0 na Al Hilal na kushinda mechi ya mwisho kwa bao 1-0 mbele ya ASAS ya Djibouti.

Al Hilal ilianza kundi B kwa kuichapa Asas mabao 2-0, kisha kuizima Red Arrows mabao 5-0 na kuinyoosha Gor Mahia kwa mabao 2-0 na kumaliza kama vinara wa kundi n pointi tisa na mabao tisa huku wavu wake haukuguswa. Ndipo ikakutana na APR katika nusu fainali na kuendelea kuonyesha ina ukuta wa chuma usiogusika kwa kucheza dakika 120 bila kufungana kabla ya kung’olewa kwa penalti 5-4.

Wababe wao, yaani APR ilitakata Kundi C kwa kuanza na ushindi bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars, kisha kuichapa Al Merrikh ya Sudan Kusini bao 1-0 na kumalizia na sare ya 1-1 dhidi ya SC Villa ya Uganda.


MWENDO WA NOTI

Kabla ya kupigwa kwa mchezo wa fainali ya michuano hiyo, mapema saa 6 mchana, Al Hilal na Al Wadi zitavaana katika mechi ya mshindi wa tatu ambaye atavuna Dola 10,000 (zaidi ya Sh26 milioni).

Tangu Rais Kagame aanze kuidhamini michuano hiyo amekuwa akiweka zawadi ya Dola 60,000 (zaidi ya Sh159 milioni) ambapo bingwa huvuna Dola 30,000 (karibu Sh80 milioni), huku ya pili inabeba Dola 20,000 (zaidi ya Sh53 milioni). Mbali na udhamini wa Kagame, michuano ya msimu huu imepigwa tafu pia na Chama cha Soka cha Sudan (SFA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Azam TV na  City College Of Health  ambayo imekuwa ikitoa zawadi kwa wachezaji bora wa kila mechi (man of the match) tangu hatua ya makundi. Hivyo, pamoja na kwamba klabu hizo zinachuana kuacha alama katika michuano hiyo, lakini zitakuwa zikipiga hesabu fedha za zawadi za udhamini a ubingwa.


MCHANA NYAVU

Wakati michuano ikifikia tamati leo, kuna nafasi kubwa kwa nyota wa Al Hilal, Mohammed Abdelrahman kumaliza kinara wa mabao kwani hadi sasa anaongoza akiwa na mabao matano. Nyota huyo anayekumbukwa na mashabiki wa Yanga alivyowakatili katika michuano ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2022-2023 kwa kuifunga nje ndani na kuifanya iangukie Kombe la Shirikisho na kufanikiwa kutinga fainali dhidi ya waliotwaa ubinhwa, USM Alger ya Algeria, alifunga mabao hayo katika mechi tatu mfululizo za makundi, kabla ya juzi kutibuliwa na APR.

Abdelrahman anafuatiwa kwa karibu na Adama Coulibaly pia wa Al Hilal, mchezaji pekee aliyefunga hat trick mwaka huu akiwa na mabao matatu, huku kukiwa na msururu wa orodha ya waliofunga bao moja moja wakiwamo Allasane Diarra na Paul Katema wa Red Arrows.

Ingawa soka huwa na maajabu yake, lakini bado Msudani ana nafasi zaidi ya kuongeza idadi ya mabao kupitia mechi ya mshindi wa tatu, huku waliopo nyuma yake wakiwa na kazi kubwa ya kufunga mabao mengi zaidi ili wampiku katika mbio za mfungaji bora wa msimu huu. Katika fainali za mwisho za Kagame 2021, wachezaji watatu akiwamo Paul Peter wa Azam FC, Muzamiru Mutyaba na Erick Kambale wote wa Express ndio walioibuka wafungaji bora kila mmoja akifunga mabao matatu.


APR NI VINARA WA MATAJI

Ushindi kwa APR utaifanya kujisogeza kwenye orodha wa vinara wa kubeba mataji mengi ya michuano hiyo kwani itafikisha la nne na kushika nafasi ya tatu nyuma ya vinara Simba na AFC Leopards ya Kenya zilizobeba mara sita kila moja.

APR imetwaa mataji mwaka 2004, 2007 na 2010, ikilingana na timu za Sudan Al Merrikh ya Sudan na SC Villa ya Uganda, huku vinara Simba ilitwaa taji mwaka 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002, wakati AFC Leopards, ilitwaa mara mbili ikitumia jina la Abaluhya mwaka 1967 na 1979 kisha kuendelea ikiwa na jina la sasa 1982, 1983, 1984 ikiwa timu pekee iliyotwaa mara tatu mfululizo kabla ya kubeba mara ya mwisho 1997.

Kwa Yanga ilibeba taji la michuano hiyo mwaka 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012, huku Gor Mahia ilianza kubeba ikifahamika kama Luo Union 1976 na 1977 kisha ikiwa na jina la sasa ikarudia tena 1980, 1981 na 1985, wakati Tusker ilibeba 1988, 1989, 2000, 2001 na 2008.

Hivyo mashabiki wa soka wanaoifuatilia michuano hiyo wana kiu ya kutaka kujua ni APR itaongeza mataji au Red Arrows itaandika historia ya kuwa timu ya kwanza nje ya Cecafa kubeba taji hilo la Kagame na katika tuzo binafsi, mchezaji gani atampiku Abdelrahman katika Mfungaji Bora mbali na zile za kipa bora, Mchezaji Bora wa michuano na timu yenye nidhamu? Tusubiri tuone!