Josiah alia na mambo matatu Mashujaa
Muktasari:
- Kauli hiyo inakuja baada ya timu hiyo kucheza mechi mbili ikishinda mmoja na kupoteza mmoja, huku ikifungwa na kufunga bao moja, matokeo ambayo yameonekana kutomfurahisha kocha huyo.
KOCHA Mkuu wa Mashujaa FC, Aman Josiah amesema matokeo waliyoanza nayo si mazuri wala mabaya sana, akieleza kuwa bado anasuka timu kutokana na ugeni wake, muda mfupi wa maandalizi na maingizo mapya kikosini.
Kauli hiyo inakuja baada ya timu hiyo kucheza mechi mbili ikishinda mmoja na kupoteza mmoja, huku ikifungwa na kufunga bao moja, matokeo ambayo yameonekana kutomfurahisha kocha huyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Josiah amesema matokeo hayo si mazuri sana akieleza kuwa anachopambania kwanza ni ushindi wakati akiendelea kusuka kikosi kutokana na maingizo mapya msimu huu.
Amesema mbali na kutengeneza muunganiko, hata yeye ni mgeni kwenye timu akieleza kuwa mwanzo wao kwenye ligi hajaridhishwa na kasi ya ushambuliaji kwenye eneo la kufunga mabao.
“Ni kweli kasi ya ufungaji mabao si nzuri, hatujaanza kama nilivyotaka na hii ni kutokana na ugeni wangu na maingizo mapya kikosini, bado hatujapata ule muunganiko ulio sawa ila kwa sasa napambania ushindi kwanza” amesema Josiah.
Kocha huyo amesema kuwa baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Fountain Gate, amefanya tathimini na nyota wake kuhakikisha mechi ya kesho Jumapili dhidi ya Mbeya City wanapata pointi tatu.
Amesema licha ya ugumu wa mchezo huo wa tatu mfululizo ugenini, lakini wamejiandaa kimbinu, kiufundi na kisaikolojia kuwakabili wenyeji hao ili kupata ushindi utakaowaweka pazuri kwenye msimamo.
“Kucheza mechi tatu mfululizo ugenini siyo tatizo kwakuwa kinachotoa matokeo ni maandalizi ndani na nje ya uwanja, tumejipanga na matarajio ni kushinda mchezo huo ili kujiweka pazuri,” amesema Kocha huyo.