JKU, ZFF kuimarisha mawasiliano
Muktasari:
- Kanali Daima alisema kwasasa dunia imehamia mitandaoni, hivyo ni wajibu kutumia nafasi hiyo kutoa taarifa kwa wakati juu ya maendeleo ya timu, hali ambayo itachangia kuvutia wadhamini na wafadhili kuwekeza.
MKUU wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU), Kanali Makame Abdallah Daima, ameahidi kuendeleza ushirikiano kati ya JKU na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) hasa kubadilishana uzoefu kupitia vitengo vya habari na masoko.
Kanali Daima alisema kwasasa dunia imehamia mitandaoni, hivyo ni wajibu kutumia nafasi hiyo kutoa taarifa kwa wakati juu ya maendeleo ya timu, hali ambayo itachangia kuvutia wadhamini na wafadhili kuwekeza.
Kanali huyo, alieleza hayo Oktoba 28, 2026 wakati akizungumza na Ofisa Habari na Mawasiliano wa ZFF, Namala Suleiman, katika Makao Makuu ya Jeshi hilo, Saatani, Unguja.
“Ni vyema ZFF kuendelea kutoa semina elekezi kuhusu habari na masoko kwa vilabu vya Ligi Kuu ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu fursa mbalimbali,” alisema Mbali na hilo, Kanali huyo aliisisitiza ZFF kuendelea kusimamia waamuzi kwenye kufuata sheria 17 za mpira ili kudumisha ushindani na kuipa hadhi Ligi Kuu.
Naye, Ofisa Habari na Mawasiliano ZFF, Namala Suleiman alisema Shirikisho limedhamiria kuzikumbusha timu zote kuweka nguvu kupitia vitengo vya habari kujiendesha wenyewe.
Namala alisema mpira unahitaji kutangazwa kupitia vyombo vya habari ili jamii ipate uelewa juu ya kinachoendelea kwenye timu zao.