Inzaghi afichua kilichomkwamisha Namungo
Muktasari:
- Namungo waliweka mezani Sh27 milioni ili kuondoka na mshambuliaji huyo, lakini viongozi wa Uhamiaji hawakuridhika na kiasi hicho cha fedha wakitaka kiongezwe.
BAADA ya Namungo kuinasa saini ya mshambuliaji wa Uhamiaji, Ali Khatibu 'Inzaghi' wameamua kuachana naye kwani hawakufikia makubaliano rasmi na viongozi wa timu hiyo.
Namungo waliweka mezani Sh27 milioni ili kuondoka na mshambuliaji huyo, lakini viongozi wa Uhamiaji hawakuridhika na kiasi hicho cha fedha wakitaka kiongezwe.
Mwanaspoti lilimshuhudia mshambuliaji huyo kwenye uwanja ambao timu hiyo wanautumia kufanya mazoezi hivyo ikamua kuzungumza naye na amesema alikuwa tayari kuondoka na Namungo na alisharidhia kiasi hicho ingawaje kwa viongozi hatambui kitu gani kilikwamisha upande wao.
"Viongozi sijui walikuwa wanataka kiasi gani na nahisi hapo ndipo waliposhindwana na hawajaniambia kilichoendelea hadi sasa," amesema, huku akiamini hiyo ndiyo safari ya utafutaji kwake ndiyo maana aliridhia kwa hiyo Sh27milioni.
"Naamini hapa kati kulikuwa na mambo ambayo yanaendelea na ndiyo yaliyofelisha mchongo wangu kwa hivyo nitaangalia dirisha dogo," amesema,
Namungo ilifunga kambi kisiwani hapa mara tu baada ya kumalizika kwa msimu wa 2025-2026 ikiwania saini ya mshambuliaji huyo na licha ya nyota huyo kumalizana nao, viongozi wa Uhamiaji waligoma kumruhusu kuondoka hadi sasa.