Kangwanda amuibua kocha Zambia
Muktasari:
- Lwandamina, ambaye pia anafanya kazi na Kangwanda katika kikosi cha Chipolopolo, amesema historia ya wachezaji waliowahi kucheza Yanga ilimfanya kuwa na hofu kama kiungo huyo angeweza kukabiliana na presha ya klabu hiyo.
KOCHA wa muda wa timu ya Taifa ya Zambia, George Lwandamina,amesema awali alikuwa na wasiwasi kuhusu Albert Kangwanda alipokwenda Yanga, lakini kiwango alichoonyesha tangu ajiunge na mabingwa hao wa Tanzania kimemfanya abadili mtazamo wake.
Lwandamina, ambaye pia anafanya kazi na Kangwanda katika kikosi cha Chipolopolo, amesema historia ya wachezaji waliowahi kucheza Yanga ilimfanya kuwa na hofu kama kiungo huyo angeweza kukabiliana na presha ya klabu hiyo.
“Nilikuwa na wasiwasi naye wakati anasajiliwa Yanga kutokana na rekodi ya waliopita kwenye timu hiyo, lakini nimebadili mtazamo wangu kwa sababu ubora wake umeimarika zaidi,” amesema Lwandamina.
Amesema pamoja na Kangwanda kuanza kuonyesha uwezo wake, bado anatakiwa kuongeza juhudi zaidi ili kuendelea kupata nafasi ya kuaminiwa na mashabiki wa Yanga. “Kwa kiwango chake cha sasa nimemwambia anatakiwa kuongeza juhudi zaidi, kwa sababu kama amekubalika na mashabiki wa Yanga basi ataweza kufanikiwa kirahisi zaidi,” amesema.
Kangwanda alijiunga na Yanga Julai mwaka huu akitokea Red Arrows ya Zambia, ambako alikuwa ametoka kuwa na msimu bora wa 2025/26 akiwa na mabao 17 na asisti tisa katika mashindano yote.
Lwandamina amesema alifurahishwa zaidi na namna Kangwanda alivyoanza safari yake Yanga baada ya kufunga kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya Simba, akiamini hatua hiyo ilimsaidia kuondoa hofu na kupata kujiamini.
“Nilifurahishwa na hatua yake ya kufunga kwenye dabi yake ya kwanza. Ninaamini hilo litakuwa limemuondoa woga na kumjengea kujiamini zaidi kwenye mchezo unaofuata naamini atafanya vizuri kuliko alivyofanya huku.”
DABI IJAYO
Mchezo mwingine wa watani hao wa jadi unatarajiwa kuwa Oktoba 10, 2026 huku Kangwanda akiwa miongoni mwa wachezaji ambao macho ya mashabiki yataelekezwa kwake kutokana na uwezo aliouonyesha kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya Simba.
Lwandamina ambaye anakumbukwa kwa makubwa aliyofanya Yanga amesema uzoefu alioupata Kangwanda kwenye dabi yake ya kwanza unaweza kuwa muhimu kwake kuelekea mchezo huo, hasa baada ya kujua aina ya presha inayotokana na mechi kubwa ya Kariakoo.
“Ninaamini uzoefu alioupata kwenye dabi yake ya kwanza utamsaidia sana kuelekea mchezo unaofuata. Tayari ameshajua presha na ukubwa wa mechi ya Kariakoo, hivyo anaweza kuingia akiwa na utulivu na kujiamini zaidi,” amesema Lwandamina mmoja kati ya makocha wakubwa Afrika.