Ibenge aona njia ya makundi CAFCC
Muktasari:
- Azam ilirejea nchini Jumamosi iliyopita kuendelea na maandalizi ya mchezo huo, ikiwa na matumaini ya kutumia vizuri faida ya kucheza nyumbani na kupata matokeo yatakayoihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika mashindano hayo.
KOCHA wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema kikosi chake kina kazi kubwa ya kufanya katika mchezo wa marudiano dhidi ya ZED FC ya Misri ili kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Azam ilirejea nchini Jumamosi iliyopita kuendelea na maandalizi ya mchezo huo, ikiwa na matumaini ya kutumia vizuri faida ya kucheza nyumbani na kupata matokeo yatakayoihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika mashindano hayo.
Ibenge amesema anashukuru kwa matokeo ya mchezo wa kwanza, lakini akasisitiza kuwa bado hawajamaliza kazi na wanapaswa kujiandaa vizuri ili kutimiza lengo la kufuzu hatua ya makundi.
“Bado tuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu. Ninashukuru kwa matokeo tuliyopata katika mchezo wa kwanza, lakini tuna kazi ya kujiandaa kwa ajili ya mchezo wa marudiano kwa sababu tunatakiwa kushinda. Hilo ndilo jambo muhimu zaidi kwetu,” amesema Ibenge.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika nchini Misri, ZED ilitangulia kupata bao kupitia Mahmoud Nabil dakika ya 45, kabla ya Iddy Nado kuisawazishia Azam dakika ya 58 na kuifanya timu hiyo kurejea nyumbani ikiwa na matumaini ya kufuzu.
Matokeo hayo yanaacha ushindani wazi kuelekea mchezo wa marudiano, ambapo Azam italazimika kutumia vizuri nafasi za kufunga huku ikiwa makini kuzuia mashambulizi ya wapinzani wake.
Kwa upande wake, ZED inatarajiwa kuingia katika mchezo huo ikiwa na lengo la kuzuia Azam kutumia faida ya kucheza nyumbani na yenyewe kutafuta matokeo yatakayoiwezesha kusonga mbele. Hali hiyo inafanya maandalizi ya timu zote mbili kuwa muhimu katika pambano hilo.
Azam inaingia katika hatua hii ikiwa na kumbukumbu nzuri ya msimu uliopita wa 2025/26, ilipofuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
Katika hatua za awali za mchujo, Azam iliiondoa El Merriekh ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0, baada ya kushinda mabao 2-0 katika kila mchezo wa nyumbani na ugenini.
Baadaye, ilikutana na KMKM ya Zanzibar na kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza, kabla ya kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao 7-0 katika mchezo wa marudiano uliofanyika Chamazi. Matokeo hayo yaliifanya Azam kufuzu kwa jumla ya mabao 9-0 na kupata tiketi ya kucheza hatua ya makundi, mafanikio ambayo sasa inalenga kuyarejea katika msimu huu.