Ibenge amtupia jicho kiungo Mkongomani
IMEELEZWA kiungo wa kati, Tenda Denis Mutuila kutoka DR Congo, yupo na kikosi cha Azam FC akiwa kwenye uangalizi wa kiwango chake ili kama Kocha Florent Ibenge ataridhishwa naye, basi atakuwa kati ya wachezaji ambao watasajiliwa dirisha dogo.
Mwanaspoti limepata taarifa za ndani za kiungo huyo, kuanza mazoezi na wachezaji wa Azam, lakini haishi katika kambi ya timu hadi pale atakapoonyesha kiwango cha kuridhisha.
Kiungo huyo aliyezaliwa Kinshasa nchini DR Congo Aprili 14, 2003 (umri wa miaka 23), amewahi kuzitumikia FC Lupopo na AS Maniema Union zote za DR Congo.
Chanzo kutoka Azam kilisema: “Pamoja na mchezaji huyo kufanya mazoezi na timu, haimaanishi tayari amekuwa na asilimia 100 za kusajiliwa, kocha Ibenge atamwangalia kama atafaa kuongeza nguvu kikosini.
“Ni kawaida kwa viongozi au benchi la ufundi, wakati ligi inaendelea kuangalia ni wachezaji gani, wanaweza wakaja kuongeza nguvu kikosini, kwani kuna timu pia ambazo zinakuwa zinaangalia wachezaji wetu na zinakuwa zinatamani kuwasajili.
“Katika usajili wa dirisha dogo lazima tutaongeza wachezaji, hivyo uwepo wa mchezaji huyo ni jambo la kawaida hadi pale kocha atakapouambia uongozi kwamba anamhitaji.”