Ibenge aitaka Union Maniema
Muktasari:
- Ibenge anataka kutumia nafasi hiyo kukipima kikosi chake dhidi ya timu ya nje ya Tanzania, huku aki-amini mchezo huo utampa nafasi ya kufanya majaribio mbalimbali na kuona uwezo wa wachezaji wake katika mazingira tofauti.
KOCHA wa Azam FC, Florent Ibenge ameomba timu yake icheze mechi ya kirafiki ya kimataifa katika kipindi hiki cha kalenda ya FIFA, huku uongozi wa klabu hiyo ukiwa kwenye mpango wa kuileta nchini Union Maniema ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ibenge anataka kutumia nafasi hiyo kukipima kikosi chake dhidi ya timu ya nje ya Tanzania, huku aki-amini mchezo huo utampa nafasi ya kufanya majaribio mbalimbali na kuona uwezo wa wachezaji wake katika mazingira tofauti.
“Nimeomba tupate mechi ya kirafiki ya kimataifa katika kipindi hiki cha FIFA. Ni muhimu kwetu kucheza dhidi ya timu kutoka nje ili kupata nafasi ya kujaribu baadhi ya vitu na kuona timu yetu ilipo,” alisema Ibenge.
Kutokana na ombi hilo la kocha huyo, Azam imeanza kuangalia uwezekano wa kuileta Union Maniema nchini kwa ajili ya mchezo huo wa kirafiki ambao ukifanikiwa utakuwa sehemu ya maandalizi ya kikosi hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti Ibenge alisema anaweza kutumia mchezo huo kuwapa nafasi wachezaji ambao hawapati dakika nyingi katika mechi za mashindano rasmi, huku pia akifanya tathmini ya mifu-mo na mipango mbalimbali ya kiufundi.
“Mechi kama hii inatusaidia kwa sababu tunapata nafasi ya kujaribu wachezaji na mfumo bila kuwa kwenye presha kubwa ya mashindano. Tunataka kutumia kipindi hiki vizuri,” alisema.
Union Maniema ni moja ya timu zinazoshiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho msimu huu, hivyo mchezo dhidi yake unaweza kuwa kipimo kizuri kwa Azam ikiwa mpango huo utakamilika.
Kwa Ibenge, ambaye anatoka DR Congo, mchezo huo pia unaweza kuwa na uzito wa kipekee kwa sababu msimu uliopita alikutana na timu hiyo katika michuano ya Kombe la Shirikisho, huku Wakongo hao wakiitandika Azam kwao mabao 2-0 na Matajiri hao wa Chamazi walilipa kisasi mchezo wa pili kwa kuwachapa bao 1-0.
Azam itacheza mechi yake ya kwanza Kombe la Shirikisho ambapo itakutana dhidi ya mshindi wa mechi kati ya ZED FC ya Misri na ASAS Djibouti Télécom ya Djibouti.