Hope City Deaf yapata matumaini Ligi ya Viziwi
Muktasari:
- Ushindi huo umeipa Hope City Deaf nafasi ya kurekebisha makosa ya mchezo wa kwanza, ambapo ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Zandeaf, kabla ya kurejea kwa nguvu na kupata ushindi mnono katika mchezo wa pili.
HOPE City Deaf imeanza kupata matumaini katika Ligi ya Viziwi Zanzibar baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Zandeaf, katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo.
Ushindi huo umeipa Hope City Deaf nafasi ya kurekebisha makosa ya mchezo wa kwanza, ambapo ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Zandeaf, kabla ya kurejea kwa nguvu na kupata ushindi mnono katika mchezo wa pili.
Abuubak Makame ndiye aliyeanza kuifungulia Hope City Deaf ukurasa wa mabao baada ya kufunga dakika ya 10, huku Omar Rashid akiongeza mabao mawili dakika ya 20 na 26 na kuiweka timu hiyo katika nafasi nzuri.
Mtwana Hassan alikamilisha hesabu ya mabao manne kwa Hope City Deaf dakika ya 54, huku Zandeaf ikifanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika ya 87 kupitia Yussuf Ali.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha wa Hope City Deaf, Rashid Yahya, alisema ushindi huo umetokana na kurekebisha makosa waliyoyafanya katika mchezo wa kwanza.
“Baada ya kupoteza mchezo wa kwanza, tulikaa chini na kurekebisha makosa yaliyokuwepo. Wachezaji walifuata maelekezo na matokeo yake tumeweza kupata ushindi,” alisema Yahya.
Alisema kikosi chake kilionesha kiwango kizuri tangu mwanzo hadi mwisho wa mchezo, jambo lililowasaidia kutumia nafasi walizopata na kupata matokeo waliyokuwa wakiyahitaji.
Ushindi huo unaipa Hope City Deaf matumaini mapya katika ligi hiyo baada ya kuanza kwa kupata kipigo katika mzunguko wa kwanza.