Hofu chanzo timu za Zanzibar kukwama
Muktasari:
- Mbali na hilo, aliwataka wachezaji wa KVZ wanaoshiriki mashindano ya Kagame Cup nchini Rwanda yanayoanza Julai 24, 2026 wapambane kwa ajili yao na Zanzibar.
MKUU wa Utawala Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ), Kanali Juma Hussein, amesema hofu ndio kikwazo kikubwa kinachozifelisha timu za Zanzibar.
Amesema, mara nyingi timu hizo zinapoteza mashindano baada ya kusikia zinacheza na timu kubwa, hivyo wao hujiona hawana uwezo wa kupambana nazo.
Ameeleza kuwa katika mashindano yoyote ukiacha hofu ichukue utawala wake ni vigumu kufanikiwa na hilo huwa sehemu mojawapo ya kushindwa.
"Kwa kawaida timu za Zanzibar zinapoteza mashindano baada ya kusikia wanacheza na timu kubwa kwa maana hiyo wanajiona wadogo hawana uwezo wa kushindana nazo," amesema Kanali Juma.
Akitolea mfano wa Kombe la Mapinduzi na Muungano, amesema sababu kubwa za timu kisiwani hapa kuishia hatua za awali wanajiona hawana uwezo wa kuifunga Yanga, Simba au Azam wakati sio kweli.
Amesema, kwa namna hiyo wachezaji na Ligi Kuu Zanzibar haiwezi kukua, hivyo ni wakati sahihi wa kuonesha utayari wa kushindana.
Amesema ili mpira wa Zanzibar ukue, wachezaji wa Zanzibar wanapaswa kuacha dhana hiyo kwa maslahi mapana ya soka kisiwani hapa.
Hivyo, amewataka wachezaji wa timu hiyo kuwa na nidhamu kwani ndio msingi wa mafanikio na wapo kwa lengo la kushindana na sio kushiriki.
Mbali na hilo, aliwataka wachezaji wa KVZ wanaoshiriki mashindano ya Kagame Cup nchini Rwanda yanayoanza Julai 24, 2026 wapambane kwa ajili yao na Zanzibar.