Hispania yabeba tena Kombe la Dunia
Muktasari:
- Tanzania U-17 iliyoshirikia fainali hizo za Dunia kwa mara ya kwanza ilifungwa mabao 3-0 na Colombia katika mechia ya robo fainali.
BAO la kujifunga la kiungo Ana Guzman wa Colombia limeisaidia Hispania kutetea taji la Fainali za Kombe la Dunia la Wanawake U-17 zilizofanyika na kumalizika leo nchini India.
Kiungo huyo anayecheza klabu ya Deportivo Pereira ya Colombia alijifunga dakika ya 82 katika harakati za kuokoa mpira na kuwalainishia kazi watetezi hao kubeba tena ndoo kwa mara ya pili.
Hispania inakuwa nchi ya pili kutwaa taji mara mbili la michuano hiyo ikiifikia rekodi ya Korea ya Kaskazini iliyobeba 2008 na 2016.
Colombia ndio iliyoitoa timu ya Tanzania Serengeti Girls katika hatua ya robo fainali. Michuano hiyo ya saba ilishuhudia pia Nigeria ikimaliza ya tatu kwa kuifunga Ujerumani kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa mabao 3-3.
Pia wachezaji watatu, Linda Caicedo wa Colombia,
Loreen Bender wa Ujerumani na Momoko Tanikawa wa Japan waliibuka vinara wa mabao kila mmoja akifunga manne.
Jumla ya mabao 95 yalifungwa katika mechi 32 za michuano hiyo iliyoanza Septemba 30 ikiwa ni wastani wa kufungwa mabao 2.97 kwa kila mechi.