Hiki hapa kinachowabeba Bacca, Mudathir Yanga
KATIKA kikosi ambacho ushindani wa namba umeanza kuwa mkali tangu kuanza kwa msimu wa 2026-2027, wachezaji wazawa wawili, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Mudathir Yahya, wameonyesha dalili za kuwa sehemu muhimu ya mipango ya Yanga chini ya Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi.
Bacca ambaye ni beki wa kati na Mudathir anayecheza nafasi ya kiungo wa kati katika ukabaji na ushambuliaji, si wageni ndani ya kikosi hicho. Walikuwepo muda mrefu wakipita makocha tofauti, lakini mwanzo wao wa msimu huu chini ya benchi jipya la ufundi unaonyesha namna wanavyoendelea kujijenga kwenye mfumo wa Mngqithi. Jambo kubwa zaidi ni kwamba nafasi zao hazijaja kirahisi.
Yanga imeongeza ushindani kupitia usajili wa wachezaji wapya wa kimataifa katika nafasi mbalimbali ambao ni Peter Shalulile (mshambuliaji), Albert Kangwanda (mshambuliaji), Cheikh Ibrahima Toure (mshambuliaji), Housseine Zakouani (winga), Stephane Aziz KI (kiungo mshambuliaji), Fred Ngoma (kiungo mkabaji) na Oumar Farouk Komara (beki wa kati), ambao tayari wamepata nafasi ya kucheza katika mechi za mwanzo za msimu.
Hali hiyo imeifanya kila nafasi ndani ya kikosi kuwa ya kupiganiwa mbali na ya kipa, lakini Bacca na Mudathir wameanza safari hiyo kwa kasi Ligi Kuu Bara kuhakikisha kikosi kinatetea taji. Pia tayari wamehusika kushinda Ngao ya Jamii, huku wakipambana kimataifa kuona Yanga inafikia malengo ya kucheza robo fainali msimu huu. Kumbuka Ngao ya Jamii na Ligi ya Mabingwa, nyota hao wamecheza kwa dakika zote tisini sambamba na nahodha, Bakari Mwamnyeto.
Bacca ndiye anayetoa picha kubwa ya mabadiliko ndani ya safu ya ulinzi ya Yanga akicheza mechi saba za mashindano yote kwa dakika zote 630.
Msimu uliopita, beki huyo wa kati alicheza mechi 22 za Ligi Kuu Bara wakati Yanga ikibeba ubingwa kwa mara ya tano mfululizo, akitumia jumla ya dakika 1,932 na kufunga bao moja. Msimu huu, licha ya ushindani mkubwa wa nafasi yake, Bacca tayari amecheza mechi zote tano za ligi, huku akifunga bao moja dhidi ya JKT Tanzania.
Hilo ni jambo linaloonyesha Mngqithi amekuwa akimwamini katika mipango yake ya ulinzi.
Sio kwamba nafasi hiyo haikuwa na ushindani. Yanga ina wachezaji wengine wanaoweza kucheza nafasi ya beki wa kati. Oumar Farouk Komara, ambaye amesajiliwa msimu huu, tayari amepewa nafasi na amecheza dakika 90 dhidi ya Fountain Gate.
Wakati huo huo, Dickson Job, ambaye msimu uliopita alicheza mechi 10 na kutumia dakika 847, alikuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha, lakini sasa amepona na kuongeza tena ushindani katika eneo hilo.
Hivyo, Bacca kuendelea kuonekana kwenye kikosi si jambo la kawaida. Ni matokeo ya kiwango na uwezo wake wa kuaminika katika mfumo wa kocha. Katika msimu uliopita Bacca alifunga bao moja na tayari msimu huu amefikisha idadi hiyo hiyo baada ya kufunga dhidi ya JKT Tanzania. Lakini umuhimu wake kwa Yanga haupaswi kupimwa kwa mabao pekee.
Kama beki wa kati, kazi yake kubwa ni kuhakikisha timu inapata utulivu nyuma, inajenga mashambulizi kutoka eneo la chini na kuifanya timu kuwa na uwiano inapokuwa na mpira.
Dakika alizocheza msimu huu zinaonyesha kwamba Bacca amepewa jukumu hilo mara kwa mara.
Kwa upande mwingine, Mudathir ameingia msimu huu akiwa na kumbukumbu nzuri zaidi ya uliopita.
Kiungo huyo alicheza mechi 22 msimu wa 2025-2026 katika Ligi Kuu Bara, akitumia dakika 1,293, akifunga mabao tisa na kutoa asisti tatu. Hizo ni takwimu zinazomweka Mudathir katika kundi la viungo waliokuwa na mchango mkubwa kwenye uzalishaji wa mabao wa Yanga msimu uliopita.
Msimu huu naye amecheza mechi zote tano za kwanza katika Ligi Kuu Bara, lakini si kama Bacca kwani ametumia dakika 308, huku tayari akiwa amefunga mabao mawili na kutoa asisti moja. Ukijumlisha na zile dakika 180 za Ngao ya Jamii na kimataifa, jumla ni dakika 488. Kwa hiyo, ndani ya mechi saba za mashindano yote, Mudathir tayari ameshafikisha zaidi ya robo ya mabao aliyofunga msimu mzima uliopita katika ligi. Hapa ndipo umuhimu wake unapojitokeza ambapo Mngqithi anamwona kama kiungo wa kazi.
Mudathir si mchezaji anayehitaji tu kuwa na mpira miguuni ili kuonekana. Anaweza kusaidia timu katika kuunganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji, kushiriki katika kujenga mashambulizi na pia kufika eneo la mwisho. Mabao tisa aliyofunga msimu uliopita yalikuwa ushahidi wa uwezo huo, wakati asisti tatu ziliongeza thamani yake kama mchezaji anayehusika moja kwa moja kwenye kutengeneza nafasi. Msimu huu, mabao mawili na asisti moja katika mechi tano yanaonyesha kuwa bado ni mchezaji muhimu zaidi. Licha ya hivyo, changamoto kubwa kwa Mudathir ni kwamba eneo la kiungo lina ushindani mkali.
Duke Abuya, ambaye msimu uliopita alicheza mechi 29 za Ligi Kuu kwa dakika 2,437, amekuwa sehemu muhimu ya kikosi, huku msimu huu tayari akiwa na mechi nne na dakika 339. Amekosa mechi moja. Kimataifa na Ngao ya Jamii pia amecheza.
Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye msimu uliopita alicheza mechi saba za Ligi Kuu Bara, naye amepewa nafasi mbili msimu huu.
Kisha kuna Fred Ngoma, mmoja wa wachezaji wapya, ambaye tayari amecheza mechi mbili na kutumia dakika 88. Hivyo, Mudathir anapambana si tu na wachezaji aliokuwa nao msimu uliopita, bali pia wale ambao wameletwa kuongeza ubora na ushindani kikosini.
WAZAWA VS WAGENI
Yanga imefanya usajili ambao umeongeza chaguo la Mngqithi katika maeneo mbalimbali.
Kangwanda tayari amefanya vizuri akiwa na mabao mawili na asisti mbili katika mechi tano, huku Toure akiwa na bao moja na asisti moja katika mechi tano za Ligi Kuu Bara zilizoifanya Yanga kukaa kileleni mwa msimamo.
Zakouani, naye ameonyesha uwezo wa kutengeneza nafasi akiwa na asisti tatu katika mechi tatu alizocheza.
Hawa ni baadhi tu ya wachezaji wapya ambao wameingia kwenye ushindani wa namba na kuwafanya wazawa kulazimika kuongeza kiwango. Lakini Bacca na Mudathir hawajapotea kwenye ushindani huo, badala yake, wameendelea kupata nafasi.
Bacca na Mudathir hadi sasa wamecheza mechi zote saba za mashindano zikiwemo. Katika hilo, pia nahodha Bakari Mwamnyeto aliyekosa mechi moja ya ligi, jumla amecheza mechi sita, nne za ligi, moja Ngao ya Jamii na nyingine Ligi ya Mabingwa.
MZIZE, JOB ITAKUWAJE?
Clement Mzize ambaye msimu uliopita alikosa mechi za ligi kutokana na majeraha ya goti, sasa amepona hivyo kurejea kwake kutaongeza machaguo ya ushambuliaji.
Kumbuka kabla ya kuumia alikuwa mchezaji muhimu wa Yanga eneo la ushambuliaji hasa msimu wa 2024-2025 alipomaliza ligi na mabao 14 akiwa kinara kikosini Yanga akizidiwa mabao mawili na kinara wa jumla, Jean Charles Ahoua aliyekuwa Simba aliyefunga 16. Pia kurejea kwa Dickson Job baada ya kupona jeraha la goti kunamaanisha kwamba eneo la ulinzi litakuwa na ushindani zaidi. Job alitengeneza pacha nzuri na Bacca.