Hii ndiyo Stars ya kwenda Kenya
Kocha wa timu ya Simba, Abdalah Kibaden ambaye ametajwa kuwa anastahili kuwa Kocha Mkuu kikosi cha timu ya taifa ya Kilimanjaro Stars, huku akisaidiwa na Juma Mwambusi wa Mbeya City na Charles Boniface Mkwasa wa Ruvu Shooting.
Muktasari:
Wadau wanajiuliza ni kwa nini Ligi Kuu Tanzania Bara isimame mwezi Novemba kupisha timu ya Taifa wakati wachezaji wanaochaguliwa wanatoka timu nne tu za Simba, Yanga, Azam na Mtibwa? Hizo ni kati ya 14 za ligi hiyo.
KOMBE la Chalenji litaanza Novemba 27 nchini Kenya na mechi zake zitachezwa hadi Desemba 14 siku ambayo bingwa wa michuano hiyo ya vikosi vya taifa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati atajulikana. Tanzania Bara itawakilishwa na Kilimanjaro Stars huku Zanzibar ikiingiza Zanzibar Heroes.
Wadau wanajiuliza ni kwa nini Ligi Kuu Tanzania Bara isimame mwezi Novemba kupisha timu ya Taifa wakati wachezaji wanaochaguliwa wanatoka timu nne tu za Simba, Yanga, Azam na Mtibwa? Hizo ni kati ya 14 za ligi hiyo.
Nimekuwa nikifuatilia Ligi Kuu Bara kwenye mechi mbalimbali kuanzia timu za mikoani mpaka za Dar es Salaam, haya ni mapendekezo yangu ya kikosi bora kinachoweza kuiwakilisha Bara katika mashindano hayo.
Nimeunda kikosi cha wachezaji 25 na makocha wanaostahili kuiongoza timu hiyo badala ya Kim Poulsen ambaye ni kocha wa Taifa Stars. Ni kwa sababu yeye ni kocha wa timu ya Muungano unaohusisha Bara na Visiwani.
Makocha
Kocha Abdalah Kibaden wa Simba anastahili kuwa Kocha Mkuu huku akisaidiwa na Juma Mwambusi wa Mbeya City na Charles Boniface Mkwasa wa Ruvu Shooting.
Makocha hao wamefanya vizuri kwenye ligi inayoendelea na wana uelewa na uhalisia wa soka la Bara. Nadhani ni wakati mwafaka wa wao kupewa majukumu, Kim anapaswa kukaa pembeni kuangalia zaidi vipaji vya Bara na Visiwani kwenye michuano hiyo pamoja na kushauri kama mtu asiyefungamana na upande wowote.
Wachezaji
Kikosi changu ni kama ifuatavyo; Makipa ni Hamis Seif (JKT Ruvu), Abdul Juma (Ruvu Shooting) na Hussen Shariff (Mtibwa). Hawa ni miongoni mwa makipa walioonyesha kiwango cha hali ya juu katika kuzuia magoli bila kujali udhaifu wa mabeki wao.
Mabeki ni Abdi Banda (Coastal Union), Kessy Mapande (JKT), Jumanne Fadhili (Prisons), George Kavila (Kagera Sugar), Samir Luhava (Ashanti), Hassan Mwasapila (Mbeya City), George Oseah (Ruvu Shooting), Dickson Daudi (Mtibwa) na David Luhende (Yanga).
Upande wa ushambuliaji ukiweka na viungo wa kati ni Paulo Maona (Ashanti United), Jonas Mkude (Simba), William Lucian (Simba), Deus Kaseke (Mbeya City), Frank Domayo (Yanga) na Juma Luizio (Mtibwa).
Wengine ni Said Ndemla (Simba), Mohamedy Hussen (Mgambo), Elvis Maguli (Ruvu Shooting), Peter Michael (Prisons), Themi Felix (Kagera), Paul Nonga (Mbeya City) pamoja na Farid Mussa Maliki (Azam).
Katika kikosi hicho kuna wachezaji wasiozidi wanne tu ambao ndio wamewahi kuitwa Stars. Timu hii haina majina maarufu, lakini ni timu iliyozingatia uwajibikaji, umri na maumbile. Dunia ya soka ndivyo inavyotaka.
Lakini ni jukumu la makocha husika kuwatengeneza wachezaji hao ili kufikia kiwango stahili kuendana na mfumo. Nina imani
kama hao watapewa jukumu hilo, wanaweza kurudi na kombe kwa vile watataka kuonyesha mambo mapya waliyonayo.
Ni ukweli usiopingika kuwa Tanzania ina wachezaji wengi mahiri na ambao wakipewa nafasi wanaweza kuonyesha kitu cha tofauti.
Meneja wa Taifa Stars, Leopard Tasso Mukebezi, alikuwa akichezea Balimi ya Kagera tena ikiwa Ligi Daraja la Pili lakini hakukosekana Taifa Stars kwa zaidi ya miaka mitano.
Si yeye tu, walikuwapo akina Manga, Ngulungu, Masha, Kinanda, Msomali na wengineo.
Kwa mtazamo huo naamini kuwa timu ya taifa si lazima iundwe na timu chache bali inatakiwa iundwe na wachezaji bora kutoka sehemu mbalimbali ili kuweka utaifa mbele. Ndio maana katika orodha yangu nimezingatia zaidi viwango kuliko ubora.
Mwandishi wa makala hii ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari pia ni kocha na mchambuzi wa soka anapatikana katika email [email protected]