Hesabu za kiungo zimamoto ZPL
Muktasari:
- Ibrahim alisema chini ya Kocha Mkuu Abdallah Mohamed ‘Bares’, mambo yamebadilika ndani ya kikosi hicho, huku mipango ya kuwania ubingwa ikiwa tayari imeandaliwa na kinachosubiriwa ni utekelezaji wake uwanjani.
KIUNGO wa Zimamoto FC, Ibrahim Ramadhan, anaamini timu hiyo ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2026-2027 kutokana na mikakati iliyowekwa na benchi la ufundi.
Ibrahim alisema chini ya Kocha Mkuu Abdallah Mohamed ‘Bares’, mambo yamebadilika ndani ya kikosi hicho, huku mipango ya kuwania ubingwa ikiwa tayari imeandaliwa na kinachosubiriwa ni utekelezaji wake uwanjani.
“Zimamoto tuna uwezo wa kubeba ubingwa msimu wa 2026-2027. Mipango imesukwa, kilichobaki ni utekelezaji ambao upo mikononi mwetu wachezaji,” alisema Ibrahim.
Aliongeza kuwa moja ya mikakati ya timu hiyo ni kukusanya pointi nyingi katika michezo ya mzunguko wa kwanza ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwania taji hilo.
Alisema Kocha Bares amekuwa karibu na wachezaji wote, akifanya kazi ya kuboresha viwango vyao pamoja na kuongeza makali ya safu ya ushambuliaji wanapokuwa uwanjani.
Ibrahim alifafanua kocha huyo amekuwa akifanya jitihada za kukijenga kikosi kuwa kitu kimoja na kupunguza presha ya ushindani wa ligi ili wachezaji wabaki kwenye malengo yao.
“Nitapambana kwa jasho na damu kuhakikisha tunatimiza malengo yetu msimu huu. Ninaamini kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu tutafanikiwa,” alisema. Zimamoto inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa na pointi 25 baada ya kucheza michezo 10, imeshinda nane, sare moja na kupoteza mchezo mmoja.