Hersi ajivunia mataji 16 Yanga
Muktasari:
- Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Yanga, Hersi alisema mafanikio hayo yanathibitisha mwelekeo sahihi wa klabu, huku akiwapongeza viongozi, benchi la ufundi, wachezaji, wanachama na mashabiki kwa ushirikiano waliouonyesha.
Rais wa Yanga na mgombea pekee wa nafasi hiyo, Injinia Hersi Said, amesema anajivunia mafanikio makubwa ambayo klabu hiyo imeyapata chini ya uongozi wake, akieleza kuwa tangu achaguliwe Julai 9, 2022, timu hiyo imetwaa jumla ya mataji 16 ya mashindano mbalimbali.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Yanga, Hersi alisema mafanikio hayo yanathibitisha mwelekeo sahihi wa klabu, huku akiwapongeza viongozi, benchi la ufundi, wachezaji, wanachama na mashabiki kwa ushirikiano waliouonyesha.
Kwa mujibu wa Hersi, mataji hayo yanajumuisha ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la CRDB, Kombe la Mapinduzi, Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano pamoja na mataji mbalimbali ya kimataifa ambayo Yanga ilialikwa kushiriki.
"Mafanikio haya ni makubwa sana kwa Yanga na tunapaswa kujivunia. Yote yametokana na uongozi imara pamoja na malengo tuliyojiwekea ya kutimiza kiu ya wanachama na mashabiki wetu," alisema Hersi.
Mbali na mafanikio ya uwanjani, Hersi alisema anajivunia pia mageuzi ya kiuongozi yaliyofanywa ndani ya klabu, akidai mfumo wa uendeshaji wa Yanga umevutia vilabu mbalimbali kutoka nje ya Tanzania kufika kujifunza namna klabu hiyo inavyoendeshwa.
Aidha, alisema katika kipindi hicho cha miaka minne, Yanga imefanikiwa kuongeza idadi ya wanachama hadi kufikia 112,000, hatua ambayo imechangia kuimarisha mapato ya klabu.
"Tumefanikiwa kusajili wanachama 112,000, jambo ambalo limeongeza nguvu ya kiuchumi ya klabu na kutuwezesha kukusanya zaidi ya Sh4.5 bilioni kupitia mfumo wa uanachama," alisema Hersi.
Alisisitiza kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya msingi wa kuifanya Yanga iendelee kuwa miongoni mwa klabu zenye ushindani mkubwa ndani na nje ya Tanzania.