Hawa Juma amtazama Naijat
Muktasari:
- Ingawa JKT Queens ilishindwa kutwaa taji hilo katika fainali, michezo hiyo imempa nafasi ya kupata uzoefu wa ushindani na kuonyesha uwezo wake.
KIPA wa JKT Queens, Hawa Juma amesema ana ndoto ya kufikia ubora wa Naijat Abbas, akimtaja kipa huyo mfano anaotaka kujifunza kutoka kwake ili kuboresha uwezo wake uwanjani.
Hawa, aliyepandishwa kikosi cha JKT Queens, amesema amekuwa akimfuatilia Naijat na kuvutiwa na namna anavyosimamia safu ya beki na kuwasiliana na wenzake na kutoa maelekezo yanayosaidia timu kuwa imara inapokuwa kwenye presha.
Ameongeza kinachomvutia zaidi ni namna Naijat anavyokuwa kiongozi uwanjani na umakini wake katika kuzuia mabao, hali inayomfanya awe na matarajio ya kufikia kiwango kama hicho siku zijazo.
AIisema anatambua bado ana kazi kubwa ya kufanya ili kufikia ubora anaoutamani, hivyo anahitaji kuendelea kujifunza na kuongeza uzoefu kila anapopata nafasi ya kucheza.
“Naijat ni kipa mzuri sana na wengi tunamtazama kama mfano, kuna vitu najifunza kutoka kwake lakini bado sijafikia ubora na sifa zake,” amesema Hawa
Kipa huyo alipata nafasi ya kuanza katika mashindano ya Ngao ya Jamii baada ya Naijat kutumikia adhabu msimu uliopita. Alianza kwa kutoruhusu bao katika ushindi wa JKT Queens wa 1-0 dhidi ya Mashujaa Queens, kabla ya kucheza pia katika fainali dhidi ya Simba Queens.
Ingawa JKT Queens ilishindwa kutwaa taji hilo katika fainali, michezo hiyo imempa nafasi ya kupata uzoefu wa ushindani na kuonyesha uwezo wake.