Prime
Hamisa Mobetto ana siri nzito kuhusu Aziz KI
Hamisa Mobetto ameacha maswali baada ya kuonekana jana, Agosti 14, katika tamasha la Imbeju Sauti Moja, lililofanyika Viwanja vya Posta Kijitonyama, akiwa peke yake bila mumewe, supastaa wa soka Stephane Aziz KI.
Kutokuwepo kwa Aziz KI katika tukio hilo kumeongeza udadisi, hasa ikizingatiwa kuwa wawili hao wamekuwa wakionekana pamoja katika matukio mbalimbali wanapokuwa Tanzania.
Mwanaspoti ilipokutana na Hamisa katika tamasha hilo na kumuuliza “Aziz KI yuko wapi?”, hakutoa jibu la moja kwa moja, badala yake akafunga mdomo kwa kidole huku akitabasamu.
Mwanaspoti ikaamua kumchimba zaidi kuhusu taarifa zinazozagaa kwamba Aziz KI ameshasajiliwa na Yanga na kwamba huenda akatambulishwa rasmi leo, siku ambayo ndiyo dirisha la usajili linafungwa, hapo pia Hamisa hakutaka kufungua kinywa chake kuhusu hilo.
Badala yake, amesisitiza kuwa hana la kusema kuhusu suala hilo na kuamua kuhamishia mazungumzo kwenda kwenye mambo mengine.
“Sifumbui mdomo wangu kuhusu hilo niache mimi,” Hamisa amesema kwa kifupi, huku akiashiria kwamba mazungumzo hayo yaendelee kwenye mada nyingine.
Kauli hiyo imeacha maswali, hasa wakati ambapo jina la Aziz KI limekuwa likitajwa kwa nguvu katika mpango wa kurejea Jangwani.
Aziz KI, ambaye aliwahi kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Yanga, aliondoka Tanzania na kujiunga na Wydad Casablanca ya Morocco 2025. Baada ya kipindi chake Wydad, alihamia klabu ya Al-Ittihad Tripoli ya Libya 2026, ambako alicheza kwa kipindi kifupi.
Taarifa za hivi karibuni zinadai kwamba Yanga imekuwa ikifanya juhudi za kumrejesha kiungo huyo Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa Agosti 14, Yanga ilipeleka ofa ya Dola 500,000 kwa Al-Ittihad kwa ajili ya Aziz KI, huku ofa hiyo ikiripotiwa kuwa na malipo ya Dola 300,000 wakati wa kusaini na Dola 200,000 nyingine baadaye.
Taarifa hizo pia zinadai Al-Ittihad imekubali pendekezo hilo, ingawa hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho bado zilikuwa zikifanyika.
Hilo ndilo linalofanya ukimya wa Hamisa kuwa na uzito zaidi.
Wakati mashabiki wa Yanga wakisubiri taarifa rasmi kuhusu kurejea kwa Aziz KI, Hamisa yuko Tanzania, lakini katika tamasha kubwa kama Imbeju Sauti Moja anaonekana bila mumewe na, zaidi ya hapo, anakutana na swali kuhusu Aziz KI na Yanga, kisha anachagua kufunga mdomo.
Aziz KI alikuwa miongoni mwa mastaa waliowahi kuacha alama Yanga kabla ya kuondoka, akicheza nafasi muhimu katika mafanikio ya klabu hiyo. Sasa, taarifa za kurejea kwake Jangwani zimeibua shauku kubwa miongoni mwa mashabiki wa Yanga, huku suala la usajili likisubiri uthibitisho rasmi wa klabu.
Kwa Hamisa, hata hivyo, jana haikuwa siku ya kutoa majibu kuhusu Aziz KI. Badala yake, tabasamu, kidole mdomoni na kauli yake ya kutotaka kuzungumzia suala hilo vimeacha siri nzito kuhusu Aziz KI, huku swali likibaki; je, Hamisa anajua kinachoendelea nyuma ya pazia kuhusu mumewe na kurejea kwake Yanga?