Hababuu aagana na KVZ
Muktasari:
- Hata hivyo, amesema anaondoka akiwa na amani kwa kuwa ameiacha timu katika mazingira mazuri bila kuwa na migogoro yoyote na viongozi wa klabu hiyo.
KVZ imeamua kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hababuu Ali baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa matokeo ya kikosi hicho katika Ligi Kuu Zanzibar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Hababuu alithibitisha kuondoka kwake, akieleza kuwa uamuzi huo umetokana na matarajio ya uongozi wa klabu hiyo ya kutaka kuiongoza ligi, tofauti na nafasi waliyonayo kwa sasa.
Hata hivyo, amesema anaondoka akiwa na amani kwa kuwa ameiacha timu katika mazingira mazuri bila kuwa na migogoro yoyote na viongozi wa klabu hiyo.
“Ni kweli KVZ imeachana na mimi baada ya kutoridhishwa na nafasi tuliyopo kwenye msimamo wa ligi hiyo,” amesema Hababuu.
Kwa sasa, KVZ inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa imecheza mechi 10, imeshinda tano, sare tatu na kupoteza mbili, huku ikiwa na pointi 18. Wakati KVZ ikiachana na Hababuu, Fufuni SC imefanya mabadiliko ya benchi la ufundi kwa kumteua Abdulmanaf Abdallah kutoka Tanga kuwa Kocha Mkuu, huku Vuai Silima akipewa jukumu la kuwa Kocha wa Makipa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Fufuni, Ame Ali amesema wameamua kufanya mabadiliko hayo ili kuimarisha kikosi na kukiweka katika mazingira mazuri ya kupambana kusalia Ligi Kuu.
Amesema timu hiyo haipo katika hali nzuri, hivyo benchi jipya la ufundi lina jukumu la kuhakikisha linaibadilisha hali ya kikosi na kukinusuru na hatari ya kushuka daraja.