Makali ya KVZ yaanza kuonekana Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- KVZ iliyoiwakilisha Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na kuondoshwa kwa jumla ya mabao 4-0 na Asswehly ya Libya, mechi ya kwanza ya ligi ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Polisi, kisha ikatoka sare ya 1-1 na JKU.
BAADA ya bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, KVZ kuanza ligi kwa kusuasua, sasa timu hiyo imeonyesha makali yake katika mechi tatu za hivi karibuni baada ya kushinda zote.
KVZ iliyoiwakilisha Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na kuondoshwa kwa jumla ya mabao 4-0 na Asswehly ya Libya, mechi ya kwanza ya ligi ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Polisi, kisha ikatoka sare ya 1-1 na JKU.
Baada ya hapo, KVZ imeshinda mechi tatu mfululizo bila ya kuruhusu bao ikitikisa nyavu za wapinzani mara tisa ndani ya dakika 270 jambo ambalo hapo awali haifanya. Imezifunga Raskazone (4- 0), Mlandege (2-0) na Fufuni (3-0).
Akizungumzia hilo, Kocha Mkuu wa KVZ, Hababuu Ali amesema baada ya kutokuwa na mwendo mzuri, wakaamua kubadili mpango wao ikiwemo kutoa nafasi kwa wachezaji tofauti tofauti hali iliyozaa matunda haraka.
Hababuu ameongeza wakati wanajiandaa na mechi hizo, waliweka mpango mkakati wa kuhakikisha wanavuna pointi tisa, jambo ambalo limefanikiwa.
Alibainisha kutokana na hilo, wachezaji wakaamua kujitoa kupambania malengo hayo na kutengeneza mfumo ambao umezaa matunda chanya.
"Wachezaji wamejitoa kwa ajili ya timu baada ya kuanza vibaya kwenye ligi, na kweli tumepata ambacho tulikuwa tunakitaka," amesema Hababuu.
Alieleza KVZ imefanya usajili kwa wachezaji wengi na wazuri ndiyo maana inafanya mabadiliko ya kikosi kila mechi kutengeneza muunganiko.
Amesema benchi la ufundi linafanya hivyo ili timu isitegemee wachezaji wachache badala yake wote wanapaswa kuwa na viwango vizuri na kuipa timu inachohitaji.
Alifafanua endapo watajenga wachezaji wachache wa kutegemewa itakuwa shida wakipata majeraha, hivyo hawataki itokee hilo ndiyo maana wanahakikisha wote wanakuwa na viwango sawa.
Matokeo hayo sasa yanaifanya KVZ katika mechi tano ilizocheza kukusanya pointi kumi ikishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ZPL, ikizidiwa pointi tano na vinara, Uhamiaji iliyoshinda mechi zote tano.