Gofu kufungua fursa mpya za ajira, biashara Serengeti
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Misana Mwishawa, akizungumza na waandishi wa habari Jumatano, Oktoba 14, 2026, katika eneo la Fort Ikoma, nje ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, lilipojengwa uwanja wa gofu unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi mwishoni mwa wiki hii.
Muktasari:
- Uwanja wa gofu wenye mashimo 18 uliojengwa Fort Ikoma unalenga kuongeza muda wa watalii kukaa Serengeti, kukuza mapato ya utalii na kufungua fursa za ajira na biashara kwa wananchi.
Serengeti. Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeanzisha zao jipya la utalii wa michezo kupitia uwanja wa gofu wenye mashimo 18, hatua inayolenga kuvutia watalii zaidi, kuongeza muda wa kukaa kwa wageni na kukuza mapato ya Serikali.
Uwanja huo uliojengwa kwa fedha za Serikali katika eneo la Fort Ikoma, nje ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Oktoba 18, 2026, na kufungua fursa mpya za utalii, ajira na biashara kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka hifadhi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano, Oktoba 14, 2026, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Misana Mwishawa, amesema uwanja huo unalenga kuongeza thamani ya utalii wa Serengeti kwa kuvutia wachezaji wa gofu kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema uwepo wa uwanja huo unatarajiwa kuwafanya baadhi ya watalii kuongeza siku za kukaa katika eneo hilo, hali itakayoongeza matumizi yao katika hoteli, usafiri na huduma nyingine za utalii.
“Lengo hasa ni kuongeza idadi ya siku za wageni kukaa katika hifadhi na maeneo mengine yaliyo karibu na uwanja huu. Tunajua kwamba ukiongeza siku za kukaa kwa watalii, tunakusanya fedha nyingi zaidi ambazo zinaongeza uchumi wa taifa letu kupitia tozo zinazotokana na shughuli mbalimbali za utalii,” amesema.
Mwishawa amesema uwanja huo una upekee wa kuwa karibu na maeneo ya uhifadhi, tofauti na viwanja vingi vya gofu vilivyojengwa mijini, jambo linalotarajiwa kuvutia wachezaji wanaotaka kuunganisha michezo na utalii wa mazingira ya asili.
Amesema wachezaji wa gofu mara nyingi hutumia fedha nyingi katika huduma mbalimbali, hivyo uwepo wa uwanja huo ni fursa ya kuongeza fedha zinazobaki nchini kupitia utalii.
“Tunajua wanaocheza gofu wengi ni watu mashuhuri na wenye uwezo, tunataka fedha zao zibaki Tanzania kupitia mchezo huu,” amesema.
Ameongeza kuwa uwanja huo umebuniwa kwa kuzingatia mazingira ya asili na una changamoto zinazoweza kuongeza ushindani na mvuto kwa wachezaji wenye uzoefu.
Mbali na mapato ya Serikali, Mwishawa amesema uwanja huo unatarajiwa kunufaisha wananchi wa vijiji vinavyozunguka eneo hilo kupitia ajira na biashara mbalimbali.
Amesema vijana walioshiriki katika ujenzi wa uwanja huo wamepata mafunzo na wanaendelea kuandaliwa ili waweze kutoa huduma kwa wachezaji watakaoutumia.
Ametaja hoteli, wasafirishaji na watoa huduma wengine kuwa miongoni mwa wanufaika watakaoweza kuongeza mapato kutokana na wageni watakaokuja kucheza gofu na kutembelea vivutio vingine vya utalii.
“Kwa mfano, mtu aliyepanga kukaa siku tatu anaweza kuongeza muda wa kukaa, hapo mwenye hoteli ananufaika, wasafirishaji wananufaika na wananchi wanaotoa huduma mbalimbali nao wanapata fursa,” amesema.
Mwishawa amesema uzinduzi rasmi wa uwanja huo unatarajiwa kufanywa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Oktoba 18, 2026.
Amesema wachezaji wa gofu kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Malawi wanatarajiwa kushiriki uzinduzi huo, hatua inayolenga kuongeza hamasa na kutangaza uwanja huo katika masoko ya ndani na kimataifa.
Pia, amesema uwanja huo utatumika kufundisha mchezo wa gofu kwa wanafunzi wa vyuo na watoto, kwa lengo la kukuza mchezo huo nchini na kuandaa wachezaji watakaoweza kushiriki mashindano ya kimataifa.
“Tunataka kutumia uwanja huu kujenga kizazi kinachopenda michezo, hususan gofu, ili baadaye tuwe na wachezaji mashuhuri watakaoshindana na wenzao duniani,” amesema.
Kuhusu uhifadhi, Mwishawa amesema hatua mbalimbali zilichukuliwa wakati wa ujenzi ili kupunguza athari kwa mazingira na wanyamapori.
Amesema mfumo wa umwagiliaji umewekwa chini ya ardhi na maji ya ardhini yanatumika kumwagilia nyasi za uwanja huo. Pia, mabwawa madogo yamechimbwa nje ya uwanja kwa ajili ya wanyamapori kupata maji.
Ameongeza kuwa eneo hilo halijawekewa uzio unaozuia wanyama kupita, ili kuhakikisha shughuli za utalii wa michezo haziathiri mienendo yao.
Amesema mafanikio ya uwanja huo yatapimwa kwa uwezo wake wa kuvutia wageni zaidi, kuongeza muda wa kukaa kwa watalii na kukuza mapato yatokanayo na shughuli za utalii.
Naye Mhandisi Enock Magire, msimamizi wa ujenzi wa uwanja huo, amesema umejengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na umetambuliwa na vyama vya gofu vya kimataifa, ikiwemo USGA na R&A.
Amesema uwanja huo una ukubwa wa ekari 450, mashimo 18 na kiwango cha jumla cha mipigo 72 (par 72), huku ukiwa na urefu wa kilomita 7.096, sawa na yadi 7,761.4.
Amesema umebuniwa kuwa na changamoto mbalimbali kwa wachezaji, zikiwemo mikunjo ya njia za kuchezea, upepo na vikwazo vingine vinavyohusiana na mchezo huo.
Kwa mujibu wa Magire, uwanja huo una miundombinu inayokidhi mahitaji ya mchezo wa gofu, ikiwemo eneo la driving range kwa ajili ya mazoezi, putting green kwa ajili ya kuboresha upigaji wa mipira kuelekea mashimoni, pamoja na mfumo wa umwagiliaji unaohudumia eneo lote.
“Uwanja wetu una viwango vya kimataifa na ndiyo maana umetambuliwa na vyama vya gofu vya kimataifa, USGA na R&A, na tayari tumepata cheti kwa ajili ya kuanza kuutumia,” amesema.
Magire amesema tofauti kubwa ya uwanja huo na mingine ni mazingira yake ya asili, ambayo yatawawezesha wachezaji kufurahia mchezo huku wakitazama mandhari ya Serengeti na wanyamapori.
“Maeneo mengine viwanja vimejengwa kwa kubadilisha mazingira ya asili, lakini hapa kila kitu unachokiona ni cha asili. Huo ndiyo upekee wa uwanja huu na utakaovutia wachezaji wengi kuja kucheza Serengeti,” amesema.