Geita Gold, Kagera Sugar zarejea Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Kagera Sugar imepanda mapema baada ya wapinzani wake wa karibu Polisi Tanzania kukubali kipigo cha bao 1-0 Mbuni FC. Kwa matokeo hayo Polisi Tanzania hata akishinda mechi zake mbili zilizobaki atafikisha pointi 66 zinaweza kuwaidia katika kwenda kucheza playoff dhidi ya timu mbili za ligi kuu.
TIMU za Geita Gold na Kagera Sugar zimerejea Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2026-2027, baada ya kujihakikishia ushindi katika mechi zao za raundi ya 28, ambapo zimezifanya kufikisha pointi ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine zozote.
Katika mechi za leo, Geita Gold imeibuka na ushindi wa mabao 3-1, dhidi ya Songea United na kufikisha pointi 71, na kuweka rekodi ya kushinda 22, sare tano na kupoteza moja, wakati Kagera Sugar ilipata tiketi ya kurejea katika ligi hiyo baada ya kuichapa KenGold ya Mbeya kwa mabao 3-0.
Ushindi huo wa Kagera Sugar umeifanya kufikisha pointi 68, ikiwa imeshinda mechi 21, sare tano na kupoteza mbili kati ya 28 iliyocheza, ikiungana na Geita Gold kurejea tena Ligi Kuu Bara, kwani timu zinazopanda moja kwa moja ni mbili tu.
Kagera Sugar imepanda mapema baada ya wapinzani wake wa karibu Polisi Tanzania kukubali kipigo cha bao 1-0 Mbuni FC. Kwa matokeo hayo Polisi Tanzania hata akishinda mechi zake mbili zilizobaki atafikisha pointi 66 zinaweza kuwaidia katika kwenda kucheza playoff dhidi ya timu mbili za ligi kuu.
Geita inayofundishwa na Kocha, Zubery Katwila ilishuka daraja msimu wa 2023-2024, ambapo ushindi huo wa leo umeifanya kufikisha pointi zake 71, ambazo zimeihakikishia kumaliza nafasi mbili za juu katika msimamo wa Ligi ya Championship.
Mara ya mwisho kwa Geita kucheza Ligi Kuu ilikuwa msimu wa 2023-2024, ikimaliza nafasi ya 15 na pointi zake 25, baada ya kushinda mechi tano, sare 10 na kupoteza 15, ikiungana na Mtibwa Sugar iliyomaliza ya 16 na pointi 21, japo imesharejea.
Mechi ya mwisho kwa timu hiyo iliyohitimisha safari yake ya Ligi Kuu Bara, ilipigwa Mei 28, 2024, ambapo ilichapwa mabao 2-0, dhidi ya Azam FC kwa mabao ya Yeison Fuentes na Feisal Salum 'Fei Toto', ikitimiza siku 740, za majonzi na furaha.
Geita Gold iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu uliopita wa 2024-2025, wa Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, ikiwa na aliyekuwa Kocha, Mohamed Muya na kushindwa kurejea Ligi Kuu, baada ya kufeli mechi za 'Play-Off'.
Timu hiyo ilicheza 'Play-Off' ya kupanda Ligi Kuu dhidi ya Stand United, 'Chama la Wana' iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudiwa ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2, kisha kuchapwa ugenini 2-0.
Kwa upande wa Kagera Sugar inayofundishwa pia na nyota wa zamani wa kikosi hicho, Juma Kaseja ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya timu hiyo kumaliza nafasi ya 15 na pointi 23, ikiungana na KenGold iliyomaliza ya 16 na pointi 16.