Gamondi aitumia salamu Super Eagles
Muktasari:
- Taifa Stars na Nigeria zitashuka dimbani kesho Ijumaa, Novemba 13, 2026 katika pambano la kusaka tiketi ya kufuzu fainali za AFCON 2027, litakalofanyika kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio, jijini Uyo.
Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Miguel Gamondi, amesema kikosi chake hakijasafiri kwenda Nigeria kuwa sehemu ya kufanikisha safari ya taifa hilo kufuzu fainali za AFCON 2027, bali kupambana kwa lengo la kupata ushindi.
Taifa Stars na Nigeria zitashuka dimbani kesho Ijumaa, Novemba 13, 2026 katika pambano la kusaka tiketi ya kufuzu fainali za AFCON 2027, litakalofanyika kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio, jijini Uyo.
Mchezo wa marudiano kati ya Taifa Stars na Super Eagles utafanyika Jumanne, Novemba 17, kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar
Akizungumza na Mwananchi kutoka Nigeria jana, Gamondi alisema kuwa, mbali na tiketi, wana kila sababu ya kutafuta ushindi ili kuboresha rekodi ya Tanzania, wachezaji mmoja mmoja na yeye kama kocha wa timu hiyo.
Alisema kuwa wanaiheshimu Nigeria, lakini hawataruhusu heshima hiyo kuwa sababu ya kushindwa kupambana kutafuta matokeo.
“Tunaijua Nigeria, tunaiheshimu na tunajua historia yake. Lakini tutaikabili kama tunatafuta nafasi ya kufuzu. Kamwe hatutaki kuwa daraja wala ngazi ya Nigeria kufikia malengo yake,” alisema Gamondi na kuongeza:
“Ushindi ni muhimu kwa Tanzania, lakini pia kwa wachezaji mmoja mmoja na kwangu kama kocha, kwa sababu utaboresha rekodi zetu.”
Aliongeza kuwa kikosi chake kina wachezaji wenye uzoefu wa kukabiliana na mechi kubwa na kwamba maandalizi yaliyofanyika yanampa imani ya kufanya vizuri.
Kauli ya Gamondi imekuja wakati Taifa Stars ikiendelea na maandalizi yake jijini Uyo, ambako ilifika Jumanne baada ya safari iliyoanzia Abuja, ilikowasili Jumatatu.
Katika mazoezi yake ya kwanza yaliyofanyika Jumanne jioni kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio, wachezaji walifanya mazoezi ya viungo, kupokezana mipira na kutumia koni chini ya usimamizi wa benchi la ufundi.
Naye Mkurugenzi wa Timu za Taifa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Almasi Kasongo, amesema Taifa Stars haina sababu ya kuiogopa Nigeria, akieleza kuwa mchezo huo ni wa dakika 90 na matokeo yanaweza kwenda kwa upande wowote.
Kasongo alisema kikosi hicho kimeandaliwa vizuri na kina wachezaji wenye uwezo wa kushindana na wapinzani wa kiwango cha juu, wakiwamo wanaocheza ndani na nje ya nchi
“Hatuogopi. Mpira ni mchezo wa dakika 90. Tunaujua ubora wa wachezaji wa Nigeria na historia yao, lakini tumejiandaa vizuri na tuna wachezaji wa ndani na wa nje wanaoweza kukabili jukumu hili,” alisema.
Nigeria inaingia katika mchezo huo ikiwa na presha ya kutafuta pointi muhimu baada ya kukusanya pointi tatu katika mechi mbili na kushika nafasi ya pili kwenye Kundi L.
Kwa upande wa Tanzania, ambayo ni mwenyeji mwenza wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda, tayari imepata tiketi ya kushiriki fainali hizo.
Guinea-Bissau ndiyo kinara wa Kundi L ikiwa na pointi sita, huku Nigeria ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu. Tanzania na Madagascar zinafuatia zikiwa na pointi moja kila moja.
Katika mchezo huo wa kwanza, Gamondi hatakuwa na huduma za wachezaji wawili wa Yanga, Clement Mzize na Dickson Job, ambao aliwaondoa katika msafara huo ili kuwapa nafasi ya kuimarisha utimamu wao wa mwili baada ya kuuguza majeraha
Kufuatia hali hiyo, kocha huyo alimuongeza kikosini winga wa Azam FC, Iddy Nado, kama mbadala wa Mzize.
Kikosi cha Taifa Stars chenye wachezaji 24 kina mchanganyiko wa nyota wanaocheza ndani na nje ya nchi, akiwamo Novatus Miroshi wa Göztepe ya Uturuki, Cyprian Kachewele wa Kryvbas ya Ukraine na Bernard Kamongo wa FC Dallas ya Marekani.
Kwa upande wa Nigeria itakosa huduma ya mshambuliaji wake nyota, Victor Osimhen, ambaye anasumbuliwa na jeraha la goti na tayari amefanyiwa upasuaji.
Kocha wa Nigeria, Éric Chelle, alitangaza kikosi cha wachezaji 24 bila Osimhen, kipa Maduka Okoye na kiungo mshambuliaji Kelechi Iheanacho.
Hata hivyo, Nigeria bado ina kikosi chenye uzoefu na wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuamua matokeo, wakiwamo Ademola Lookman, Moses Simon, Akor Adams, Tolu Arokodare, Alex Iwobi na nahodha Wilfred Ndidi.
Katika mazoezi yao ya kwanza yaliyofanyika Jumanne jioni, wachezaji 17 pekee kati ya 24 walishiriki, huku wengine wakitarajiwa kujiunga na kikosi baada ya kukamilisha safari zao.
Hali hiyo inaifanya mechi hiyo kuwa kipimo muhimu kwa timu zote mbili, huku Taifa Stars ikitaka kuthibitisha kuwa inaweza kushindana na vigogo wa Afrika na Nigeria ikisaka matokeo yatakayoiwezesha kufuzu AFCON 2027.