Fikiri: Simba, Yanga zimetujenga
Muktasari:
- Coastal Union imekuwa na mwanzo wa kusuasua katika Ligi Kuu Bara msimu huu, ikiwa na pointi saba baada ya kucheza mechi sita, ikishinda mbili, kutoka sare moja na kupoteza tatu. Katika mechi hizo, Wagosi wa Kaya wamefunga mabao sita na kufungwa manane.
KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Fikiri Elias amesema mapumziko ya ligi yamewapa nafasi ya kurejea mazoezini na kurekebisha mifumo ya timu, huku akisisitiza kuwa wamejenga ujasiri baada ya kukutana na vigogo Simba na Yanga mw anzoni mwa msimu.
Coastal Union imekuwa na mwanzo wa kusuasua katika Ligi Kuu Bara msimu huu, ikiwa na pointi saba baada ya kucheza mechi sita, ikishinda mbili, kutoka sare moja na kupoteza tatu. Katika mechi hizo, Wagosi wa Kaya wamefunga mabao sita na kufungwa manane.
Kikosi hicho kilianza msimu kwa kupoteza bao 1-0 dhidi ya Mashujaa, ikafungwa 4-1 na Yanga, kabla ya kutoka sare ya 1-1 na TRA United na kupoteza 1-0 dhidi ya Simba. Baadaye ilipata ushindi wake wa kwanza kwa kuifunga Polisi Tanzania 2-1, kabla ya kuichapa JKT Tanzania kwa matokeo kama hayo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fikiri alisema kikosi chake kilirejea mazoezini Jumatatu ya wiki hii, ambapo kipaumbele kikubwa wamekiweka katika kuimarisha mifumo ya uchezaji ili Coastal Union iwe timu yenye ushindani zaidi katika michezo inayofuata.
“Tumerejea mazoezini Jumatatu ya wiki hii, kikubwa tunachokifanya ni kutengeneza mifumo ya timu ili iweze kuwa na ushindani zaidi.”
Fikiri alisema mbali na mazoezi, wameanza pia kutumia mechi za kirafiki kama sehemu ya kuwaandaa wachezaji na kuboresha viwango vyao, hasa wale ambao hawajapata muda wa kutosha kucheza katika mechi za ligi.
“Tumeshacheza mechi moja ya kirafiki ambayo ilikuwa maalum kwa ajili ya kuwapandisha kiwango cha utimamu wa mwili wachezaji ambao walikuwa hawapati muda wa kucheza kwenye ligi,” alisema.
Aliongeza kuwa bado hawajaishia hapo, kwani wamepanga kucheza mechi nyingine kesho, huku mipango ikiwa ni kuongeza michezo miwili zaidi jijini Dar es Salaam iwapo maandalizi yataenda kama walivyopanga kabla ya kukutana na Azam FC.
“Tutacheza mechi nyingine kesho na baada ya hapo, kama mambo yatakwenda vizuri, tutakuja kucheza mechi nyingine mbili jijini Dar es Salaam kabla ya kucheza na Azam.
“Hatua ya kucheza na Simba na Yanga imetujenga. Hatuna hofu na mechi kubwa za namna hiyo, tunaziheshimu timu hizo na sasa tunajiandaa vizuri zaidi,” alisema Fikiri.
Coastal Union tayari imeshakutana na timu kubwa msimu huu, ikikabiliwa na Yanga na Simba katika raundi za mwanzo. Ilifungwa 4-1 na Yanga Agosti 20, kisha ikapoteza 1-0 dhidi ya Simba Agosti 27.
Coastal Union inatarajiwa kukutana na Azam FC Oktoba 8, 2026 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, ikiwa ni moja ya mechi zitakazowapa nafasi Fikiri na kikosi chake kupima maendeleo ya maboresho wanayoyafanya wakati huu wa mapumziko.