Echesa amuua shabiki Yanga
Kocha msaidizi wa Simba, Matola akiteta jambo na kipa Juma Kaseja wakati wa mechi ya Ligi kuu kati ya watani wa jadi Simba na Yanga. Simba ilishinda 4-3.
.Mgosi asababisha mwingine azimie Mwandishi Wetu SHABIKI maarufu wa Yanga mkoani Mtwara, Suleiman Hamis Kutoboa amefariki dunia jana Jumatatu asubuhi katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara Ligula baada ya kuanguka mara baada ya kiungo, Hillary Echesa kuifungia Simba bao la nne juzi Jumapili. Lakini shabiki mwingine wa Yanga, Hamis Dakota alizimia jijini Dar es Salaam baada ya Mussa Hassan Mgosi kuifungia Simba bao la tatu. Katika tukio la Mtwara, mtoto wa marehemu, Hamis Suleiman Kutoboa alithibitisha kutokea kwa kifo cha baba yake aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara tangu juzi Jumapili jioni. Alisema walikuwa wakitazama pambano hilo la watani wa jadi kupitia kituo cha televisheni cha Star tv, na mara baada ya Hillary Echesa kufunga bao la nne na la ushindi kwa Simba, Mzee Kutoboa alianguka chini na wakamkimbiza hospitali. Hamisi alisema mazishi ya baba yake yatafanyika leo Jumanne katika kijiji cha Mbuo mkoani humo. Mmoja wa marafiki wa karibu wa marehemu, Yahaya Mussa Bure alisema Mzee Kutoboa alifariki baada ya kupandwa na presha mara baada ya Echesa kufunga bao hilo la ushindi kwa Simba. "Mzee Kutoboa ametutoka. Tulikuwa tunafuatilia mpambano wa Simba na Yanga katika kituo cha Star TV na mara baada ya Echesa kufunga bao la nne alianguka chini akatoa ulimi nje. Leo asubuhi (Jana Jumatatu) amefariki dunia na sasa tupo msibani. Madaktari wanasema chanzo cha kifo chake ni presha," alisimulia. Marehemu alikuwa mnazi mkubwa wa Yanga na alikuwa akifahamika kijijini hapo kutokana na mapenzi kwa klabu hiyo ya Jangwani. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Steven Buyoya alipoulizwa kwa simu jana, alisema; "Sipo ofsini kwa sasa, nipo njiani, nitafuatilia tukio hilo na kukujulisha baadaye." Katika tukio jingine, Hamis Dakota jijini Dar es Salaam alikimbizwa katika Hospitali ya Temeke baada ya Mgosi kufunga bao la tatu kwa kichwa. Rafiki wa Dakota, Jerry Koto alisema mara baada ya bao hilo, walimkimbiza Dakota katika Hospitali ya Temeke, ambako alipewa mapumziko ya saa tatu kabla ya kuruhusiwa kurudi nyumbani. "Ameruhusiwa kurudi nyumbani, ana matatizo ya presha, kila mara tunamzuia asiende mpirani, lakini hataki, alizimia baada ya Mgosi kufunga bao la tatu," alisema Jerry. Ni mechi ambayo mashabiki wengi walidhani ingeisha kwa sare ya mabao 3-3, lakini dakika ya 92, Echesa alifunga kwa shuti kali la umbali wa mita kama 25 na kumfanya kipa Obren Curkovic ashindwe la kufanya.