Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dube aipeleka Yanga mezani

UWEZEKANO wa Prince Dube kuchezea moja ya timu zilizopeleka ofa mezani kwa Azam ambazo ni Simba na Al Hilal ya Sudan una ugumu kama atasimamia alichowaambia marafiki zake wa karibu.

Jana, Azam ilitangaza kupokea ofa kutoka kwa klabu hizo mbili na imeziruhusu kuendelea na mazungumzo na mchezaji huyo aliyeandika barua hivi karibuni kutaka kusitisha mkataba na timu hiyo ya Chamazi, lakini yenyewe ikamkomalia ikitaka afuate masharti ya mkataba.


Mmoja wa marafiki wa karibu wa staa huyo aliyerudisha mpaka nyumba na vifaa vyote vya Azam, ameiambia Mwanaspoti kwamba baada ya kusikia ofa hizo mbili mchezaji huyo hajaonyesha kuvutiwa na inaonekana akili yake iko sehemu tofauti, ingawa lolote linaweza kutokea.


Habari zinasema kwamba akili ya staa huyo pamoja na watu wanaomsaidia inaonekana iko zaidi kwa Yanga ambayo anaisubiri ipeleke ofa mezani na baadhi ya klabu za nchini kwao Zimbabwe ikiwemo Highlanders.


"Dube hitaji lake kwa hapa nchini ni Yanga na anaamini itapeleka ofa mezani kuhitaji huduma yake na kinyume na hapo amepanga kujiunga na timu ambayo iko nje ya Tanzania. Kwa Simba wanahitajika kumshawishi sana ili abadilishe mawazo na kujiunga nayo, vinginevyo sio jambo rahisi," kilisema chanzo hicho na kuongeza kuwa Yanga wako tayari kuweka mezani Sh510 milioni ambalo ndilo dau Azam ililomsainishia Dube mwaka jana wakati anaongeza mkataba.


Azam wanakomaa wanataka Sh700 milioni na wanasema Simba na Al Hilal wamekidhi matakwa bila kufafanua kwa undani.

Inaripotiwa kuwa uongozi wa Simba upo tayari kulipa kiasi cha Dola 300,000 ambacho Azam FC inakitaka ili kumuachia Dube na upo tayari pia kumlipa mshahara ambao nyota huyo anahitaji ili iweze kumnasa na kuimarisha safu ya ushambuliaji ambayo kwa sasa inaongozwa na Freddy Michael na Omar Jobe.


"Azam inathibitisha kwamba imepokea ofa kutoka vilabu viwili tofauti vikimhitaji mchezaji wetu Prince Dube, raia wa Zimbabwe. Ofa hizo zimetoka katika vilabu vya Simba ya Tanzania na Al Hilal ya Sudan. Uongozi unazifanyia tathmini ofa hizo ili kuona ipi inafaa. Aidha, Azam FC inavikaribisha vilabu vingine kuleta ofa zao kwani milango bado iko wazi," ilifafanua taarifa ya Azam FC ingawa Mwanaspoti inajua mchezaji huyo ameshawaambia mpaka viongozi kwamba hatakwenda kwenye klabu hizo mbili.

KANUNI ZINASEMAJE
Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, mawakili Alhaji Majogoro na Iddy Monday wamesema kuwa pamoja na Azam kukaribisha ofa mezani, mwenye uamuzi wa mwisho wa wapi akacheze ni Dube mwenyewe kwa vile hawezi kupelekwa timu ambayo haridhii kuichezea.


Wamesema iwapo Simba, Al Hilal au klabu nyingine ambayo itakubaliwa na Azam kumchukua Dube, itatakiwa kufanya mazungumzo binafsi na mchezaji huyo na ikiwa itashindwa kufikia muafaka maana yake hataweza kujiunga nayo hata kama iliafikiana na klabu inayomuuza.


"Mchezaji hawezi kulazimishwa kwenda sehemu asiyoitaka. Kinachoweza kufanyika ni mchezaji kutimiza mahitaji ya mwajiri wake ili yeye awe huru kwenda anapotaka," amesema Wakili Majogoro.


Wakili Monday amesema: "Ukishasaini mkataba unakuwa mali ya klabu husika. Wao watasikiliza ofa kubwa ila mchezaji ana haki ya maslahi yake. Kama watashindwana maslahi binafsi na timu husika anaweza kukataa kwenda akachagua pengine.


"Lazima kuwe na balansi baina ya klabu inayomiliki mchezaji kupata inachotaka kwa kuzingatia thamani ya mchezaji na mchezaji mwenyewe kupata maslahi anayotaka timu anayokwenda kulingana na thamani yake."
 

Kanuni ya 59 (2) ya Ligi Kuu Bara inalazimisha klabu kufanya makubaliano binafsi na mchezaji kabla ya kumsajili hata kama klabu inayommiliki mchezaji husika imeridhia kumuuza.


"Klabu inayotaka kumsajili mchezaji aliyesajiliwa au aliye na mkataba uliobakisha muda zaidi ya miezi sita (6) na klabu nyingine, italazimika kuafikiana na klabu yake kuhusu uhamisho wake kabla ya kukubaliana na kumsajili mchezaji huyo. Klabu inawajibika kuheshimu masharti ya msingi ya mkataba wa mchezaji wa klabu nyingine," inafafanua kanuni hiyo.


KUONEKANA MSIMU UJAO
Kama Dube atachukuliwa na timu ya hapa nchini, maana yake atalazimika kusubiri hadi msimu ulimalizike ili aweze kujiunga nayo, lakini kinyume na hapo hataweza kwani hakidhi vigezo vya kikanuni kutumika msimu huu kwa vile tayari ameshaitumikia Azam FC.


"Mchezaji wa kulipwa ambaye mkataba wake umekwisha kabla ya kipindi cha usajili anaweza kusajiliwa nje ya kipindi cha usajili, TFF itahitaji kujiridhisha juu ya kuaminika kwa hali nzima ya kumalizika huko kwa mkataba na maombi mapya ya usajili yanayokusudiwa, hali hii haitamhusu mchezaji ambaye mkataba wake umesitishwa au umevunjwa," inafafanua kanuni ya 66(2).