Droo ya CAF yampa mzuka Mkongomani
Muktasari:
- Katika droo hiyo iliyopangwa juzi Jumatano jijini Cairo, Misri, Singida imepangwa kundi C na timu za AS Maniema Union ya DR Congo, Red Arrows ya Zambia na mshindi kati ya CR Belouizdad ya Algeria au AS Douanes ya Mauritania.
KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, Mkongomani Papy Kimoto, amesema amefurahia kupangwa kundi moja la Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya waajiri wake wa zamani AS Maniema Union ya kwao DR Congo.
Katika droo hiyo iliyopangwa juzi Jumatano jijini Cairo, Misri, Singida imepangwa kundi C na timu za AS Maniema Union ya DR Congo, Red Arrows ya Zambia na mshindi kati ya CR Belouizdad ya Algeria au AS Douanes ya Mauritania.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kimoto amesema kupangwa kundi moja na AS Maniema Union kunarejesha kumbukumbu nzuri wakati akiwa na timu hiyo msimu uliopita wa 2025-2026.
“Ninashukuru kukutana na timu niliyowahi kuifundisha, kwa sababu tuna kumbukumbu nzuri tulizoziweka pamoja, ni kundi gumu kutokana na aina ya wapinzani tunaoenda kukutana nao, ila naamini tutafanya vizuri na kwenda robo fainali.” amesema Kimoto.
Aidha, Kimoto amesema baada ya timu hiyo kuishia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2025-2026, kwa sasa malengo ni kuivuka hatua hiyo na kuandika rekodi nyingine mpya kimataifa na kikosi hicho. “Tuna zaidi ya mwezi mmoja kujiandaa vizuri na isitoshe tunaendelea na mashindano ya ndani ambayo yanatupa mwelekeo mzuri kabla ya kufikia huko, kundi letu ni nzuri na gumu hivyo, ni lazima tujipange ipasavyo,” amesema Kimoto.
Kimoto aliyejiunga na Singida Aprili 10, 2026, aliifundisha AS Maniema Union kwa takriban miaka minne, kuanzia mwaka 2022 hadi 2026, huku mafanikio yake makubwa ni kuifikisha hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara ya kwanza msimu wa 2025-2026.
Kocha huyo amejiunga na Singida akiwa na uzoefu wa kutosha wa kufundisha soka kwa ngazi ya klabu alioupata kwa kuzinoa timu tano tofauti za DR Congo, ambazo ni AS Maniema Union, OC Renaissance, FC Saint-Eloi Lupopo, JS Kinshasa na AS Dragons.
Msimu uliopita wa 2025-2026, Singida iliishia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa kundi C na CR Belouizdad, AS Otoho na Stellenbosch FC.