Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dar City yaanza kwa kishindo ‘Road to BAL’, kazi ipo kwa Namuwongo!

Muktasari:

  • Ushindi huo wa tofauti ya pointi 20 umeipa timu hiyo ya Tanzania mwanzo mzuri katika harakati zake za kusaka nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye jukwaa kubwa la mpira wa kikapu barani Afrika

DAR CITY imeanza vyema safari yake ya kuwania tiketi ya kushiriki michuano ya Basketball Africa League (BAL) 2027 baada ya kuichapa Ferroviario da Beira ya Msumbiji kwa pointi 96-76 katika mchezo wa mashindano ya Elite 16 Division East, yanayoendelea jijini Nairobi, Kenya.

Ushindi huo wa tofauti ya pointi 20 umeipa timu hiyo ya Tanzania mwanzo mzuri katika harakati zake za kusaka nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye jukwaa kubwa la mpira wa kikapu barani Afrika.

Hata hivyo, pamoja na ushindi huo mnono, Dar City inapaswa kujiandaa kwa mtihani mwingine mkubwa itakapokutana na Namuwongo Blazers ya Uganda katika mchezo wake unaofuata wa hatua ya makundi utakaopigwa leo Novemba 24, kuanzia saa 9:00 Alasiri kwenye Ukumbi wa Kasarani Indoor Arena.

Katika mchezo dhidi ya Ferroviario, Dar City haikuanza vizuri kama ilivyotarajiwa, kwani wapinzani wao walionyesha ushindani mkubwa katika robo ya kwanza na kuimaliza wakiwa mbele kwa pointi 25-22.

Lakini hali ilibadilika katika robo ya pili, ambapo Dar City iliongeza kasi ya mashambulizi, ikafanikiwa kupata pointi 28 dhidi ya 16 za Ferroviario na kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa pointi 50-41.

Baada ya hapo Dar City ilionekana kuudhibiti mchezo, ikitumia vizuri nafasi za kufunga na kuendelea kuongeza tofauti ya pointi katika robo mbili zilizobaki kabla ya kuhitimisha mchezo kwa ushindi wa 96-76.

Nyota wa Dar City, Jean-Jacques Boissy, alikuwa katika kiwango bora akifunga pointi 29, akikusanya rebounds tisa na kutoa assists sita, huku Nisre Zouzoua naye akionyesha makali yake kwa kufunga pointi 26.

Wawili hao walikuwa na mchango mkubwa katika ushindi huo, hasa katika eneo la ushambuliaji, ambako uwezo wao wa kutengeneza nafasi na kutumia vizuri mashuti ya nje uliiweka Ferroviario katika wakati mgumu.

Kwa upande mwingine, Youssou Ndoye aliongeza nguvu katika mchezo wa ndani kwa kufunga pointi 12 na kukusanya rebounds 12, jambo lililosaidia Dar City kuwa na ushindani.

Ushindi huo haupaswi kuifanya Dar City kutokufanya marekebisho katika maeneo mbalimbali ikiwemo kupoteza mipira kwani ilipoteza mipira mara 12 jambo ambalo benchi la ufundi linapaswa kuyafanyia kazi kabla ya mchezo unaofuata.


NAMUWONGO MTIHANI UNAOFUATA

Baada ya kuichapa Ferroviario katika mchezo wa kwanza, sasa macho na nguvu za Dar City zinaelekezwa kwa Namuwongo Blazers ya Uganda, ambayo nayo imeanza mashindano kwa ushindi baada ya kuichapa Dolphins ya Botswana kwa pointi 78-62.

Dar City itatakiwa kuingia kwenye mchezo huo ikiwa imejipanga vizuri kwa kufanyia kazi makosa waliyofanya kwenye mchezo wa kwanza.

Namuwongo ina wachezaji wenye uwezo wa kuleta madhara katika eneo la ushambuliaji, akiwamo Johnathan Jordan aliyefunga pointi 16 dhidi ya Dolphins mchezaji ambaye Dar City inapaswa kumtazama zaidi kutokana na uwezo wake wa kushambulia, Adonis Filer aliyepata pointi 14 na Makhtar Gueye aliyefunga pointi 12 hawa wakiwa na uwezo a kupata pointi kwa mashuti ya nje.

Eneo lingine linalopaswa kumfanya kocha wa Dar City, Mamadou Guèye, kuongeza umakini ni rebounds.

Namuwongo ilikusanya rebounds 51 dhidi ya Dolphins, idadi inayoonyesha uwezo wake wa kupambana chini ya kapu. Hivyo, Dar City italazimika kuongeza umakini katika rebounds za kujihami ili kuzuia wapinzani kupata nafasi nyingine za kufunga baada ya mashuti ya kwanza.

Kwa Dar City, silaha kubwa bado inaweza kuwa Boissy na Zouzoua, ambao wameonyesha uwezo wa kuiongoza timu katika ufungaji licha ya kuwa mafanikio hayatategemea nyota hao pekee, bali namna kikosi kizima kitakavyoshirikiana katika kushambulia na kujilinda.


DAR CITY INATAKA ZAIDI YA USHINDI

Kwa kuutazama matokeo ya mchezo wa kwanza, Dar City ilionesha kuwa ina uwezo wa kushindana na timu nyingine katika hatua hii ya Elite 16.

Lakini mchezo dhidi ya Namuwongo utakuwa kipimo muhimu zaidi kwa kikosi hicho, hasa namna kinavyoweza kukabiliana na timu yenye nguvu katika rebounds na uwezo wa kushambulia kwa kasi.

Mfumo wa mashindano unaelekeza timu mbili zitakazomaliza nafasi za kwanza na ya pili katika kila kundi zitafuzu hatua ya nusu fainali itakayochezwa Novemba 28, 2026. Washindi wa nusu fainali watajihakikishia tiketi ya kucheza BAL 2027, huku nafasi nyingine ya kufuzu ikitolewa kwa timu bora iliyomaliza nafasi ya tatu kati ya Division East na Division West.


MATOKEO MECHI ZA JANA

Dolphins BC 62-78 Namuwongo Blazers

Patriots 77-72 Munali Suns

Nairobi City Thunder 83-81 Urunani


MECHI ZA LEO

Ferroviaro v Dolphins BC 6:30 Mchana

Urunani v Patriots 11:30 Jioni

Munali Suns v Nairobi City Thunder 2:00 Usiku