Dar City vitani kuisaka BAL 2027
Muktasari:
- Mchezo huo utapigwa Kasarani Indoor Arena kuanzia saa 11:00 jioni ukiwa ni mwanzo wa safari muhimu kwa Dar City ambayo inalenga kuiwakilisha tena Tanzania katika ligi kubwa ya mpira wa kikapu Afrika.
MABINGWA wa Tanzania kwenye mchezo wa Kikapu, Dar City, leo Jumatatu Novemba 23, 2026, wanatarajiwa kuanza rasmi kampeni yao ya kusaka tiketi ya kucheza msimu wa 2027 wa Basketball Africa League (BAL), watakapokabiliana na Ferroviário da Beira ya Msumbiji katika mchezo wa kwanza wa Kundi B la mashindano ya Road to BAL 2027 Elite 16, yanayofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Mchezo huo utapigwa Kasarani Indoor Arena kuanzia saa 11:00 jioni ukiwa ni mwanzo wa safari muhimu kwa Dar City ambayo inalenga kuiwakilisha tena Tanzania katika ligi kubwa ya mpira wa kikapu Afrika.
Dar City inaingia kwenye mashindano hayo ikiwa na uzoefu wa kushiriki BAL kwa mara ya kwanza mwaka 2026 na ilifanikiwa kufika hatua ya robo fainali kabla ya kutolewa na Petro de Luanda ya Angola.
Uzoefu huo unaweza kuwa silaha muhimu kwa kikosi cha kocha Mamadou “Pabi” Guèye katika harakati za kutafuta mafanikio mengine ya kimataifa.
Katika kujiandaa na mashindano hayo, Dar City imeongeza nguvu kwenye kikosi chake kwa kuwasajili nyota wenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa, akiwemo Jean-Jacques Boissy nyota kutoka Senegal, ambaye aliwahi kutwaa tuzo ya MVP wa BAL mwaka 2025 akiwa na Al Ahly Tripoli, pamoja na mshambuliaji Tyler Bey huku ikiendelea kuwa na huduma ya nyota wa Ivory Coast, Nisre Zouzoua, kwa wazawa bado ina nyota wake wenye uzoefu akiwemo Hasheem Thabeet, Amin Mkosa Juma MVP wa Taifa Cup 2026 pamoja na Ally Faraj Abdallah.
Hautakuwa mchezo mwepesi kwa Dar City licha ya kuwa na historia ya kushinda katika mechi mbili za mwisho ilipokutana na Ferroviário da Beira kwani nayo ina wachezaji wazuri na wazoefu kwenye mashindano ya kimataifa na wenye uwezo wa kufunga akiwemo Joshua Thomas, Ke’Tarrious Bouchum na Ayad Munguambe.
Hivyo, Dar City italazimika kuwa makini katika ulinzi, kudhibiti rebounds na kuzuia wapinzani kupata nafasi rahisi za kufunga.
Historia nzuri dhidi ya wapinzani hao inawapa nguvu Dar City kuelekea mchezo huo. Katika michezo miwili iliyorekodiwa kati ya timu hizo katika mashindano ya mwaka 2025, Dar City ilishinda kwa pointi 87-78 na 92-77. Dar City inapaswa kushinda mchezo huo ili kujitengenezea nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata ya mashindano hayo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Amini Mkosa Juma, amesema hawategemei mchezo kuwa mwepesi kwani kila timu imebeba dhamana ya kuwakilisha nchi, hivyo wakiwa na bendera ya Tanzania watapambana kuitetea nchi na kupata ushindi na kujiweka kwenye nafasi nzuri katika mashindano.
“Benchi letu la ufundi limetuandaa vizuri kuelekea mashindano hayo, hatupo hapa kuiwakilisha Dar City pekee bali nchi nzima ya Tanzania, tutahakikisha tunaitetea vyema nchi yetu, mashabiki waliopo Kenya wajitokeze kwa wingi kutupa hamasa ili tuweze kufanya vizuri,” amesema.
Ameongeza kuwa, wanafahamiana vizuri na kiu yao kubwa ni kufuzu kucheza BAL, hivyo kutokana na sajili zilizofanywa na benchi la ufundi lilivyo waandaa ushindi kwao ni lazima
“Kwa upande wa timu yetu kulingana na maandalizi tuliofanya kwa muda mrefu na yenye hadhi ya mashindano, sajili zilizofanywa na uchaguzi wa wachezaji tulionao pamoja na ubora wa benchi letu la ufundi, hatuna sababu ya kutokushinda kwani ni muhimu sana kwa kutuweka sawa na mechi zijazo, ari ya timu kwa ujumla ni kubwa, zaidi ni kuhakikisha furaha na matarajio ya Watanzania yanafikiwa kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Dar City ipo kundi B, pamoja na Ferroviario, NAM Blazers na Dolphins BC, huku kundi A likiundwa na Urunani, Nairobi City, Munali Suns na Patriots BC.
Mfumo wa mashindano unaelekeza timu mbili zitakazomaliza nafasi za kwanza na ya pili katika kila kundi zitafuzu hatua ya nusu fainali itakayochezwa Novemba 28, 2026. Washindi wa nusu fainali watajihakikishia tiketi ya kucheza BAL 2027, huku nafasi nyingine ya kufuzu ikitolewa kwa timu bora iliyomaliza nafasi ya tatu kati ya Division East na Division West.