CRDB yazindua ‘Supa Cup’ msimu wa sita
Muktasari:
- Uzinduzi wa mashindano hayo umefanyika katika Viwanja vya John Merlini, Mkoani Dodoma, ukihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino,Janeth Mayanja, aliyekuwa Mgeni Rasmi, pamoja na viongozi wa Benki ya CRDB, wakiwemo Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Godfrey Rutasingwa, na Mkurugenzi wa Uendeshaji Huduma za Kibenki, Admin Mwansasu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Supa Cup.
BENKI ya CRDB imezindua rasmi mashindano ya Supa Cup, msimu wa sita, yanayowakutanisha wafanyakazi wa Benki kutoka Tanzania, Burundi na DR Congo kushindana katika michezo ya mpira wa miguu na mpira wa pete, kwa lengo la kuimarisha umoja, mshikamano na ustawi wa wafanyakazi.
Uzinduzi wa mashindano hayo umefanyika katika Viwanja vya John Merlini, Mkoani Dodoma, ukihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino,Janeth Mayanja, aliyekuwa Mgeni Rasmi, pamoja na viongozi wa Benki ya CRDB, wakiwemo Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Godfrey Rutasingwa, na Mkurugenzi wa Uendeshaji Huduma za Kibenki, Admin Mwansasu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Supa Cup.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mayanja amesisitiza umuhimu wa michezo katika kujenga afya bora, nidhamu na mshikamano miongoni mwa wafanyakazia. Amehimiza washiriki kutumia mashindano hayo kama fursa ya kuimarisha ushirikiano, kuheshimiana na kudumisha ushindani wenye nidhamu, huku akitambua mchango wa Benki hiyo katika kukuza ustawi wa wafanyakazi wake.
Supa Cup ni sehemu ya juhudi za Benki hiyo katika kuimarisha ustawi wa wafanyakazi kwa kuwapatia fursa ya kushiriki katika shughuli za michezo zinazochochea afya, kuimarisha mahusiano na kukuza ari ya kufanya kazi kwa pamoja. Kupitia mashindano ya mpira wa miguu na mpira wa pete, wafanyakazi wanapata nafasi ya kuonesha vipaji na uwezo wao katika mazingira yanayojenga furaha, mshikamano na roho ya ushindani.
Akizungumzia umuhimu wa mashindano hayo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki hiyo Godfrey Rutasingwa, ameeleza kuwa Benki inaendelea kutambua wafanyakazi kama nguzo muhimu ya mafanikio yake, hivyo kuwekeza katika ustawi wao ni sehemu ya kujenga mazingira bora ya kazi na kuongeza ufanisi. Ameeleza kuwa michezo kama Supa Cup inatoa fursa ya kuimarisha mahusiano, kukuza ari ya kazi na kujenga utamaduni wa kufanya kazi kama timu.
Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji Huduma za Kibenki wa Benki ya CRDB na Mwenyekiti wa Kamati ya Supa Cup, Admin Mwansasu, ameeleza kuwa mashindano hayo yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wafanyakazi wa Benki katika nchi zote tatu. Amesisitiza umuhimu wa washiriki kuonesha ushindani wenye nidhamu, kuheshimu wapinzani na kudumisha umoja kwa lengo la kupata mafanikio ya pamoja.
Kupitia ushiriki wa wafanyakazi kutoka Tanzania, Burundi na DRC, Supa Cup inaendelea kuimarisha mahusiano ya kikazi na kijamii baina ya wafanyakazi wa Benki ya CRDB katika nchi hizo