Simba yamshtaki Fadlu FIFA ikimdai fidia
Muktasari:
- Fadlu aliachana na Simba mara baada ya mchezo wa raundi ya kwanza ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United uliochezwa nchini Botswana, Septemba 2025.
Simba imemfungulia kesi ya madai Kocha Mkuu mpya wa Yanga, Fadlu Davids, shauri ambalo limefikishwa mbele ya Idara ya Sheria ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Katika madai hayo, Simba inataka Fadlu ailipe fidia klabu hiyo kwa kuvunja mkataba uliokuwepo baina ya pande hizo mbili, Septemba mwaka jana.
Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na FIFA kwenda kwa Fadlu na Simba, shauri la pande hizo mbili limepangwa kusikilizwa Januari mwakani.
FIFA imetoa nafasi kwa upande wa Fadlu kuwasilisha nyaraka na taarifa muhimu katika usikilizaji wa shauri hilo na imesisitiza kuwa, kutofanya hivyo hakutozuia shauri kufanyiwa kazi.
Fadlu aliachana na Simba mara baada ya mchezo wa raundi ya kwanza ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United uliochezwa nchini Botswana, Septemba 2025.
Katika mchezo huo, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Mara baada ya kuachana na Simba, Fadlu Davids alijiunga na Raja Casablanca ya Morocco ambayo aliitumikia hadi Juni 11, 2026 alipoonyeshwa mlango wa kutokea kufuatia mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika mashindano tofauti.
Hata hivyo, Ijumaa Novemba 6, 2026 alitangazwa rasmi kuwa Kocha Mkuu wa Yanga akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Manqoba Mngqithi.