Coastal Union, TRA United zashindwa kutambiana Mkwakwani
Muktasari:
- TRA United ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 27 lililofungwa na mshambuliaji raia wa Nigeria, Ani Prince Elijah likiwa ni la kwanza kwake msimu huu, akimalizia pasi ya kiungo Mganda, Joseph Akandwanaho.
TIMU za Coastal Union na TRA United, zimeshindwa kutambiana katika mechi kali na ya kuvutia ya raundi ya tatu ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2026-2027, baada ya miamba hiyo kutoka sare ya kufungana bao 1-1 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
TRA United ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 27 lililofungwa na mshambuliaji raia wa Nigeria, Ani Prince Elijah likiwa ni la kwanza kwake msimu huu, akimalizia pasi ya kiungo Mganda, Joseph Akandwanaho.
Nyota huyo amefunga bao hilo ambalo ni la kwanza kwake katika Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2026-2027, tangu alipojiunga na kikosi hicho na kutambulishwa Agosti 4, 2026, baada ya kuachana na Police FC ya Rwanda aliyomaliza nayo mkataba.
Bao hilo lilidumu kwa dakika 10 tu, baada ya Shiza Kichuya kuisawazishia Coastal Union dakika ya 37, kufuatia makosa ya beki wa kati wa TRA United, Mkenya Shariff Majabe kupiga mpira vibaya wakati akitaka kuuokoa.
Licha ya mashambulizi mbalimbali kwa timu zote mbili, lakini mechi hiyo ya kuvutia kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo ilishindwa kupata mbabe, ambapo hadi dakika 90, zimeshuhudia zikigawana pointi moja baada ya sare ya kufungana bao 1-1.
Matokeo hayo yanaifanya Coastal Union kucheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara bila ya ushindi msimu huu, baada ya kuanza kwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Mashujaa FC, Agosti 15, 2026, kisha kuchapwa mabao 4-1 na Yanga, Agosti 20, 2026.
Kwa upande wa TRA United haijashinda pia mechi yoyote kati ya tatu ilizocheza, baada ya kuanza na sare ya bao 1-1, dhidi ya JKT Tanzania, Agosti 16, 2026, kisha kuchapwa mabao 2-1 na matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, Agosti 20, 2026.
Kwa maana hiyo, katika mechi tatu ambazo timu zote zimecheza, Coastal Union imepata sare moja na kuchapwa mbili, ikiwa nafasi ya 14 na pointi moja, huku TRA United ikitoka sare mbili na kupoteza moja, ikishika nafasi ya 11 na pointi mbili.
Kutokana na matokeo hayo, imeifanya Coastal Union kuendeleza rekodi mbovu dhidi ya TRA United kwani kikosi hicho cha 'Wagosi wa Kaya', hakijawahi kushinda katika mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara zilizokutana tangu msimu wa 2023-2024.
TRA United ambayo zamani iliitwa Tabora United, tangu ianze kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024, imekutana na Coastal Union mara saba, ambapo kati ya hizo imeshinda moja, huku mechi sita kwa miamba hiyo ikishuhudiwa ikiisha kwa sare.
Kabla ya leo, mara ya mwisho timu hizi kukutana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, zilifungana bao 1-1, Februari 1, 2026, ambapo Coastal ilifunga kupitia penalti ya Shiza Kichuya dakika ya 35, kisha Denis Nkane akaisawazishia TRA United dakika ya 48.