Clara Luvanga mkali wa dabi
Muktasari:
- Tangu alipojiunga na Al Nassr msimu wa 2023-2024 akitokea DUX Logrono ya Hispania, Luvanga amekuwa mmoja wa wachezaji wanaoleta tofauti katika mechi zinazokutanisha vigogo hao wa soka la wanawake Saudi Arabia.
KAMA kuna mechi ambazo mshambuliaji wa Al Nassr, Clara Luvanga, anazipenda zaidi kuliko nyingine, basi ni dabi ya Saudia dhidi ya Al Hilal.
Tangu alipojiunga na Al Nassr msimu wa 2023-2024 akitokea DUX Logrono ya Hispania, Luvanga amekuwa mmoja wa wachezaji wanaoleta tofauti katika mechi zinazokutanisha vigogo hao wa soka la wanawake Saudi Arabia.
Dabi hizo zimekuwa kama eneo lake la kuonyesha ubora zaidi, akifunga mabao muhimu na mara kadhaa kugeuza mechi hizo kuwa jukwaa lake binafsi.
Kwenye mechi 10 za dabi, Luvanga amefunga mabao 17 zikiwemo hat-trick tatu na kuwa mmoja wa wachezaji wa kigeni kufunga mabao mengi kwenye michezo hiyo.
Hat-trick ya kwanza aliifunga Machi 26, 2026, katika ushindi wa mabao 4-1, ulioisaidia Al Nassr kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
Mei 21, 2026, katika fainali ya SAFF Women’s Cup iliyochezwa Kingdom Arena, Al Nassr ilikutana tena na Al Hilal, timu hiyo ilishinda 3-2 na kutwaa ubingwa, huku dabi hiyo ikiendelea kuthibitisha kwa nini jina la Luvanga limekuwa likihusishwa na mechi hizo zenye presha.
Septemba 5, 2026 katika fainali ya Super Cup, Luvanga alifunga hat-trick nyingine na kuisaidia Al Nassr kushinda 4-1 dhidi ya Al Hilal akiongeza rekodi yake ya kuwa mchezaji anayeng’ara zaidi timu hizo zinapokutana.
Akizungumzia hilo, Luvanga amesema anafurahia zaidi anapofunga katika mechi za dabi, akieleza kuwa ni michezo yenye hisia na ushindani.
“Nawashukuru wenzangu kwa mchango wao lakini pia kocha Aziz kwa kuendelea kunipa nafasi ya kuendelea kuniamini kubeba mataji ni ndoto ya kila mchezaji na naamini tutaendelea kufanya vizuri,” amesema Luvanga na kuongeza.
“Nafurahia zaidi ninapofunga kwenye dabi kwa sababu ni miongoni mwa michezo yenye hisia tofauti. Kuna ushi ndani wa aina yake unapokutana na timu hizo, hivyo kufunga na kusaidia timu yangu kushinda huwa ni jambo la furaha zaidi.”