Prime
Chama, Phiri waigawa Simba
CLATOUS Chama na Moses Phiri wameonekana kuipasua Simba kwa baadhi kutaka waendelee kuwapo klabuni huku wengine wakisema waondoke zao.
Awali, ilielezwa kuwa baadhi ya wadau wa klabu hiyo wakiwamo baadhi ya viongozi na benchi la ufundi, walitaka ishu za wachezaji hao zimalizike haraka kwa kuwaacha waende zao, lakini imeonekana kizuizi ni mikataba yao.
Hivi karibuni ilitolewa taarifa ya kusimamishwa kwa Chama, huku Phiri ikielezwa ameandika barua ya kuomba kuondoka kwenye timu hiyo kutokana na kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Hata hivyo, chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba kinasema kila kikao kinachohusu ishu hiyo, kimekuwa kikiwagawa wajumbe baadhi wakitaka wachezaji hao wabaki na wengine wakitaka waondoke.
Taarifa zinasema, Phiri bado yupo kwenye kikosi akiendelea na ishu zake kama kawaida, huku suala la Chama likiwa linasubiri Kamati ya Nidhamu kuimaliza, huku chanzo kikisema barua bado haijafikia kamati.
“Kwa Phiri hakuna ishu kwa kuwa hata klabu haijawahi kuzungumza jambo lolote kuhusu suala lake na hata sisi hatujawahi kuona hiyo barua, labda kama watu waliamua tu kuzusha ndiyo maana hata mchezo wa mwisho alikaa kwenye benchi na mazoezini hajawahi kukosa.
“Ishu ya kukosa nafasi ni ya mchezaji mwenyewe, anatakiwa kupambana, sasa kama utaona mchezaji anakosa nafasi anaomba kuondoka huyo siyo mpambanaji, inachotakiwa ni yeye kuonyesha juhudi na kila mmoja anamuamini Phiri kuwa ni mchezaji mzuri, nafikiri hata kwenye Mapinduzi ataonekana, ingawa kwa hali ya kawaida anaonekana hana furaha na amekuwa akiwatumia watu kutaka kuondoka.
“Chama kwenye Mapinduzi ana asilimia ndogo sana, kwanza haendi mazoezini na anaonekana anawaza maisha nje ya Simba, lakini shida ni kwa kuwa ana mkataba hadi mwisho wa msimu Simba hawawezi kumuacha kwa kuwa atalipwa fedha nyingi, lakini ofa ikitoka nje hata sasa naona atauzwa tu,” kilisema chanzo.