BASATA yaibua mwelekeo mpya kwa MC na waandaaji wa matukio
Muktasari:
- Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza kufanyika Novemba 23 na 24, 2026, katika Kituo cha East Africa Commercial and Logistics Centre (EACLC), Ubungo, jijini Dar es Salaam, yakihusisha washiriki wapatao 70 kutoka kada mbalimbali za tasnia ya sanaa na burudani.
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limeibua mwelekeo mpya katika tasnia ya uratibu na uandaaji wa matukio nchini baada ya kuwanoa watangazaji wa shughuli mbalimbali (MC) na waandaaji wa matukio kupitia mafunzo yaliyolenga kuongeza weledi, ubora na ufanisi katika sekta hiyo.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza kufanyika Novemba 23 na 24, 2026, katika Kituo cha East Africa Commercial and Logistics Centre (EACLC), Ubungo, jijini Dar es Salaam, yakihusisha washiriki wapatao 70 kutoka kada mbalimbali za tasnia ya sanaa na burudani.
Washiriki walitoka katika makundi ya MC, maafisa utamaduni, maafisa habari, waandaaji wa matukio, mapromota, kampuni za usimamizi wa matukio pamoja na wadau wengine wa sanaa.
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Amosi Mazaba, amesema kukua kwa sekta ya matukio nchini kunaongeza umuhimu wa kuwa na watu wenye ujuzi wa kutosha katika kupanga, kuratibu na kusimamia shughuli hizo.
Amesema mafunzo hayo yamelenga kuongeza ujuzi wa washiriki, kuimarisha mifumo ya usimamizi, kuwajengea uelewa kuhusu sheria na miongozo inayosimamia sekta hiyo, pamoja na kuwapa maarifa ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa matukio.
“Ukuaji wa sekta ya matukio nchini unaongeza umuhimu wa kuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kutosha katika kupanga, kuratibu na kusimamia shughuli hizo. Kupitia mafunzo haya tunalenga kuongeza ujuzi wa washiriki, kuimarisha mifumo ya usimamizi, kuwajengea uelewa kuhusu sheria na miongozo inayosimamia sekta hii, pamoja na kuwapa maarifa ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa matukio,” amesema Amosi Mazaba.
Naye aliyewahi kuwa mjumbe wa bodi ya BASATA Jessica Mshana, amezungumzia umuhimu wa sekta hiyo kuwa haipaswi kutazamwa kama eneo la burudani pekee, bali pia kama fursa ya kiuchumi.
"Tunapaswa kuitazama sekta ya matukio si kama eneo la burudani pekee, bali pia kama chanzo muhimu cha ajira, biashara, uwekezaji na mapato kwa wananchi na taifa kwa ujumla," alisema Mshama.
Katika mafunzo hayo, washiriki wamepata mada mbalimbali zilizowasilishwa na wataalamu kutoka sekta tofauti, zikiwemo itifaki na mwenendo wenye heshima katika uratibu wa matukio.
Mada Itifaki na mwenendo wa heshima katika uratibu wa matukio iliyowasilishwa na Balozi Omar Kashera Mjegwa, amesema misingi ya itifaki pale mtu anapojitambulisha anapaswa kutaja jina lake bila kuambatanisha cheo, kwa kuwa cheo hutajwa na mtu mwingine, ametoa mfano kuwa badala ya kusema, "Jina langu ni Engineer Salum Mpalange," ni sahihi kusema, "Jina langu ni Salum Mpalange."
"Kila wakati huwa napenda kusisitiza umuhimu wa kuendelea kujifunza na elimu haina mwisho na mafunzo haya yanatoa nafasi ya kujenga na kuboresha uwezo wa waratibu na waendesha matukio nchini, hivyo misingi ya itifaki pale mtu anapojitambulisha inapaswa kutaja jina lake bila kuambatanisha cheo, kwa kuwa cheo hutajwa na mtu mwingine," amesema Kashera
Mada nyingine ilihusu ulinzi wa taarifa binafsi katika matukio, iliyotolewa na Innocent Mungy; fursa za biashara, ujasiriamali na maendeleo ya soko katika sekta ya matukio, iliyowasilishwa na Martin Mwambene kutoka Mamlaka ya Bandari; pamoja na uwekezaji na usimamizi wa fedha, iliyotolewa na Lydia Godaina kutoka UTT.
Washiriki pia walijifunza kuhusu uratibu wa itifaki katika matukio ya kitaifa kupitia mada iliyowasilishwa na Jacob Msekwa, Mkurugenzi wa Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
Aidha, Dk Garvin Kweka kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili aliwasilisha mada ya akili hisia katika usimamizi wa matukio, akieleza umuhimu wa kuelewa na kusimamia hisia katika mazingira ya kazi.
Kwa mujibu wa BASATA, awali ilitarajia kupata washiriki kati ya 30 na 50, lakini idadi iliongezeka hadi kufikia takribani 70 waliojiandikisha na kulipia ada ya Sh 350,000.
Ada hiyo ilihusisha ushiriki wa mafunzo, vifaa vya kujifunzia, chai ya asubuhi, chakula cha mchana na chai ya jioni.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa wa BASATA, Lilian Shayo, amesema matarajio ya baraza hilo ni kuona mafunzo yakichangia kuboresha ubora wa matukio, kuimarisha usalama wa wasanii na washiriki, kupunguza changamoto zinazoweza kuzuilika na kuongeza fursa za ajira pamoja na kujiajiri.
Aliongeza kuwa BASATA ina mpango wa kuendeleza mafunzo ya aina hiyo kwa awamu nyingine zitakazofika katika kanda na mikoa mbalimbali nchini ili kuwafikia wadau wengi zaidi.
Kwa hatua hiyo, mafunzo hayo yanalenga kuimarisha weledi kwa MC na waandaaji wa matukio, ambao wana nafasi muhimu katika kuhakikisha shughuli za sanaa na burudani zinafanyika kwa mpangilio na viwango vinavyotakiwa.