Prime
Barker kusafisha nyota watatu wa kigeni
UONGOZI wa Simba umeanza kufanyia kazi mapendekezo yaliyowasilishwa na kocha mkuu, Steve Barker huku ripoti yake ikipendekeza kufanyika kwa maboresho ya kimkakati yatakayolenga kuifanya timu hiyo kuwa imara zaidi ndani na nje ya Tanzania.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa miongoni mwa mapendekezo makuu yaliyowasilishwa na Barker ni kuachana na baadhi ya wachezaji wa kigeni ambao hawajaonyesha kiwango kinachokidhi mahitaji ya benchi la ufundi.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, wachezaji watatu wa kigeni waliopendekezwa kuondolewa ni Naby Camara, Jonathan Sowah na Alassane Kante ambaye yeye anaweza kuuzwa. Hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa usajili mpya ambao utaongeza ushindani na ubora wa kikosi hicho kuelekea msimu ujao.
Chanzo hicho kilifafanua kuwa kila mmoja wa wachezaji hao ana sababu tofauti zilizochangia kuorodheshwa katika ripoti hiyo. Kwa upande wa Kante, inaelezwa nafasi yake inaweza kuzibwa na mchezaji wa ndani ambapo Simba imemalizana na Kelvin Nashon ambaye kwa sasa anaitumikia Pamba Jiji.
Nashon ambaye ni mchezaji wa Singida Black Stars atakuwa mchezaji huru baada ya msimu kumalizika na taarifa zinasema ameshasaini Simba miaka miwili.
Kwa Sowah sababu kubwa inayotajwa ni mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati yake na klabu, hali iliyomuweka nje ya mipango ya timu kwa kipindi kirefu na kuathiri mchango wake ndani ya kikosi.
Camara naye ameonekana kushindwa kuendana na mfumo wa mchezo anaoutaka Barker. Inaelezwa kocha huyo anahitaji mchezaji mwenye kasi zaidi, nguvu na uwezo mkubwa wa kukaba ili kuongeza ubunifu katika eneo la ushambuliaji.
“Camara ameshindwa kuendana na mbinu za kocha katika nafasi zote mbili, kiungo na hata beki. Kwa sasa wanatafuta mchezaji mwingine ambaye ataweza kuongeza ushindani na kumsaidia Clatous Chama katika eneo la kutengeneza nafasi za mabao. Kocha amesisitiza anahitaji mchezaji mwenye umri mdogo na nguvu zaidi,” kimesema chanzo hicho.
Mbali na kuwaondoa wachezaji hao watatu, Simba tayari imeanza kufanya kazi ya kusaka nyota wapya wa kigeni. Taarifa zinaeleza kuwa klabu hiyo inahitaji angalau wachezaji watatu wa kigeni katika maeneo muhimu ambayo yameonekana kuwa na upungufu.
Miongoni mwa nafasi zinazotafutiwa suluhisho ni mshambuliaji wa kati mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao pamoja na kiungo mshambuliaji ambaye ataongeza ubunifu katika eneo la mwisho la uwanja pamoja na kiungo mkabaji mmoja.
Hata hivyo, mbali na maingizo hayo, viongozi wa Simba kwa kushirikiana na benchi la ufundi wanaendelea kufuatilia maendeleo ya afya ya Mohammed Bajaber ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha na kama hadi mwisho wa msimu hatakuwa fiti wanaweza kuachana naye.
“Kama Bajaber atarejea kwa wakati na kuwa katika hali nzuri ya ushindani, basi atarudishwa kwenye mfumo na kuwa msaada na kama hali yake itaendelea kuwa hivi basi wataingia sokoni tena ili kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho na staa huyo wa Kenya atapelekwa kwa mkopo sehemu. Barker ana imani kubwa na uwezo wake na anaamini bado ana nafasi kubwa ndani ya mipango yake,” kimeongeza chanzo hicho.
Katika maboresho hayo, Simba pia imeelekeza nguvu katika kuimarisha safu ya ulinzi. Licha ya kuwa na mkongwe Shomari Kapombe pamoja na David Kameta ‘Duchu’, benchi la ufundi linaona kuna haja ya kuongeza ushindani katika nafasi ya beki wa kulia.
Inaelezwa kuwa tayari klabu hiyo imefikia hatua nzuri katika mchakato wa kumsajili Nathaniel Chilambo kutoka Azam FC ili kuongeza chaguo katika eneo hilo.
Upande wa kushoto wa ulinzi nao upo kwenye mipango ya maboresho ambapo Simba inatafuta beki mwenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja, hususani beki wa kushoto na kiungo mkabaji, jambo ambalo litatoa uhuru mkubwa wa kiufundi kwa benchi la ufundi.
Wakati huohuo, viongozi wa Simba wanaendelea kufuatilia mwenendo wa kipa Djibrilla Kassali kutokana na uwepo wa Moussa Camara ambaye aliondolewa kwenye mfumo kufuatia kusumbuliwa na majeraha, wataangalia wanasaliwa na nani kati ya hao au wataingia tena sokoni.
Chanzo hicho kilieleza kuwa katika usajili wa wachezaji wa kigeni, Barker amepewa mamlaka makubwa ya kufanya uamuzi ya kiufundi huku viongozi wakihusika zaidi katika masuala ya usajili wa wachezaji wazawa.
Ripoti hiyo pia imependekeza baadhi ya wachezaji wazawa ambao wamekosa nafasi ya kucheza waende kwa mkopo katika timu nyingine ili kupata muda wa kutosha wa kucheza na kuendelea kukuza viwango vyao.
Katika hatua nyingine, Simba imeanza mazungumzo ya kumbakisha Neo Maema ambaye amekuwa akiitumikia timu hiyo kwa mkopo kutoka Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Inaelezwa Barker ameridhishwa na mchango wa kiungo huyo na anaamini uzoefu wake bado unahitajika ndani ya kikosi hicho. Maema mwenyewe pia ameonyesha nia ya kuendelea kubaki Msimbazi iwapo makubaliano yatafikiwa kati ya pande husika.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL), alithibitisha kuwa uongozi umepokea ripoti ya kocha na tayari umeanza kuifanyia kazi.
“Tunajipanga kuhakikisha baada ya msimu kumalizika tunafanya maboresho yatakayokifanya kikosi chetu kuwa bora zaidi. Kazi ya kutekeleza mapendekezo ya kocha tayari imeanza na tunaendelea na tathmini katika maeneo mbalimbali,” amesema Magori.
TAKWIMU ZA BARKER SIMBA
Tangu Barker aanze kuinoa Simba, ameiongoza timu hiyo katika jumla ya mechi 27 za mashindano yote. Kati ya hizo, mechi 20 zimekuwa za Ligi Kuu Bara ambapo ameiongoza Simba kushinda mechi 13 na kutoka sare saba bila kupoteza mchezo wowote wa ligi.
Katika Kombe la CRDB, Barker ameifikisha Simba hatua ya nusu fainali baada ya kushinda mechi nne huku ikisubiri kuvaana na Coastal Union katika pambano la kusaka tiketi ya fainali.
Aidha, katika Kombe la Muungano, Simba ilishinda mechi zote tatu ilizocheza na kutwaa ubingwa, jambo lililoongeza matumaini kwa mashabiki kuwa kocha huyo anaweza kuijenga timu yenye ushindani mkubwa zaidi katika misimu ijayo, lakini pia akiwa hajapoteza mchezo wowote dhidi ya Yanga msimu huu.
KOCHA APIGA MSUMARI
Kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr amesema anaamini kama timu hiyo itaingia sokoni na kusajili wachezaji wapya wawili hadi watatu wa daraja la juu wanaweza kuendelea kufanya vizuri zaidi haswa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao. “Simba tayari wana msingi mzuri wa kikosi na hilo linaonekana wazi kabisa kutokana na namna wanavyocheza, kitu kikubwa ambacho wanaweza kufanya sasa ni kuongeza wachezaji wawili au watatu wa kiwango cha juu kwenye maeneo muhimu,†amesema.
Kerr kwa sasa yupo Marekani alikuwa kocha wa Simba msimu wa 2014/15 ambapo timu hiyo ilimaliza msimu ikiwa nafasi ya tatu ikiwa na pointi 47, nyuma ya Azam iliyokuwa na pointi 49 na Yanga ambayo ilitwaa ubingwa ikiwa na pointi 55.