KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker amebaini wachezaji wake hawezi kucheza kwa kasi ileile kwa dakika 90, jambo analohitaji kulifanyiwa kazi kwa haraka.
Simba inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 30 baada ya kushinda mechi zake 10, huku ushindi wake wa karibuni ulikuwa wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo, Novemba 2.
Kocha Barker alisema ameshtukia kupungua kwa nguvu na pumzi kwa baadhi ya wachezaji wake wanapokuwa uwanjani, hali inayoweza kuathiri uwezo wao wa kuhimili ushindani kwa dakika zote za mchezo.
Kocha huyo alisema kipindi hiki cha mapumziko ya Fifa atakitumia kuongeza utimamu wa mwili wa wachezaji ili kuhakikisha wanakuwa na nguvu za kutosha, hususan katika kipindi hiki ambacho ushindani wa ligi unazidi kuongezeka.
“Nataka kuona wachezaji wakiongeza uwezo wa kucheza kwa kasi na kuhimili presha ya wapinzani bila kupoteza nguvu kabla ya mchezo kumalizika.
“Tumegundua kuna kitu kinapungua kwa wachezaji wetu, hasa kwenye pumzi na uwezo wa kuendelea kucheza kwa nguvu. Hili ni eneo ambalo tunahitaji kulifanyia kazi tunaporejea mazoezini,” alisema Barker.
“Pamoja na mapungufu hayo, nimeridhishwa na namna kikosi kinavyopambana kupata matokeo, ingawa bado kuna maeneo yanayohitaji maboresho ili timu iwe bora zaidi, kwa sababu tunakwenda kucheza mechi ngumu baada ya mapumziko,” alisema Barker.
Pamoja na matokeo hayo, changamoto ya kudumisha kiwango kwa dakika zote za mchezo imeendelea kuwa eneo muhimu la kuangaliwa na benchi la ufundi, hasa baada ya Simba kuonyesha katika baadhi ya mechi kuwa inaweza kupata wakati mgumu inapokutana na presha ya wapinzani.
Simba inatarajiwa kuweka kambi fupi ya mazoezi nchini Kenya kupisha mapumziko ya Ligi Kuu ili kupisha mechi za kalenda ya FIFA ya mwezi Novemba 2026. Wakati wakiwa nchini Kenya, Simba SC inatarajiwa kushuka dimbani jijini Nairobi tarehe 15 Novemba 2026 kucheza mechi kirafiki dhidi ya miamba ya soka ya nchi hiyo, Gor Mahia FC.
Kwa upande wa ratiba, kabla ya kucheza dhidi ya Orland Pirates, vinara hao wa Ligi Kuu Bara Simba watacheza dhidi ya JKT Tanzania, Novemba 21, 2026, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar.