Baraza: Sio rahisi kuanza na vigogo
Muktasari:
- Pamba Jiji imeanza msimu kwa kucheza dhidi ya Dodoma Jiji na kutoka sare ya bao 1-1, kisha ikachapwa 2-1 na Simba ikaja kupokea kichapo kama hicho mbele ya Azam, huku kesho Ijumaa ikitarajiwa kukabiliana na Yanga.
KOCHA wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema ratiba yao kukutana na vigogo wa Ligi Kuu Bara mwanzoni mwa msimu ni ngumu, lakini amewapongeza wachezaji wake walivyopambana.
Pamba Jiji imeanza msimu kwa kucheza dhidi ya Dodoma Jiji na kutoka sare ya bao 1-1, kisha ikachapwa 2-1 na Simba ikaja kupokea kichapo kama hicho mbele ya Azam, huku kesho Ijumaa ikitarajiwa kukabiliana na Yanga.
Akizungumza wakati wa mazoezi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kujiandaa kuikabili Yanga uwanjani hapo, Baraza alisema kukutana na timu kubwa mfululizo ni changamoto, lakini pia ni kipimo kizuri.
“Kwanza niwapongeze vijana wangu. Ratiba haikuwa rahisi maana tumeanza na Dodoma halafu tunakutana na timu kubwa tatu, Simba, Azam na Yanga. Hawa ni vigogo, hivyo si jambo rahisi kucheza nao mwanzoni mwa msimu,” alisema.
Kocha huyo alisema pamoja na ugumu wa ratiba hiyo, Pamba Jiji imefunga bao katika kila mchezo, jambo analodai ishara kwamba kuna kitu kizuri kinajengeka.
“Nimefurahishwa na vijana wangu kwa sababu katika mechi hizi tatu tumepata bao. Hii inaonyesha kuna kitu kinatengenezwa. Wachezaji wakishikana vizuri na wale waliokuwa hawapo wakirejea katika hali nzuri ya utimamu wa mwili, naamini tutakuwa bora zaidi,” alisema Baraza.
Alisema anaamini Pamba Jiji inaweza kupata matokeo mazuri katika michezo ijayo baada ya wachezaji kuendelea kuzoea mfumo na kurejea katika kiwango kizuri cha utimamu.
“Tukirejesha ‘fitness’ yetu vizuri naamini mabao na pointi zitapatikana. Wachezaji wangu wanaendelea kuzoea mfumo haraka na hilo likiendelea itakuwa rahisi zaidi kwetu kupambana katika michezo inayofuata.”