Aziz KI avunja ukimya ishu yake Yanga, aanika usajili wa Dube

Muktasari:

  • Aziz KI amesema msimu ujao atakuwa ndani ya Yanga kuhakikisha anawasaidia washambuliaji kuwania tuzo ya ufungaji bora.

KIUNGO wa Yanga, Stephane Aziz KI, amevunja ukimya juu ya yeye kuendelea kusalia ndani ya kikosi hicho, huku akifichua jambo kubwa kumuhusu straika Mzimbabwe, Prince Dube aliyekuwa akiitumikia Azam.

Aziz KI amesema msimu ujao atakuwa ndani ya Yanga kuhakikisha anawasaidia washambuliaji kuwania tuzo ya ufungaji bora.

KI amebainisha kwamba, katika kuwasaidia washambuliaji hao, mmoja kati yao ni Dube, hivyo ni wazi straika huyo atavaa uzi wa kijani na njano msimu ujao akiachana na ule wa rangi nyeupe na bluu akiondoka katika viunga vya Chamazi.

Kauli hiyo ya Aziz Ki inaweza kuwa njema zaidi kwa Wanayanga ambao kwa muda mrefu wamekuwa na sintofahamu baada ya kuwepo kwa taarifa za kiungo huyo kuwa njiani kuondoka kutokana na mkataba wake kumalizika, huku furaha zaidi ikiwa ni baada ya kupata uhakika wa kiasi fulani juu ya uhamisho wa Dube ambaye pia anawaniwa na Simba.

Hayo yamejiri wakati Aziz KI alipokuwa akizungumza na Meneja wa Kitengo cha 'Digital' Yanga SC, Priva Abiudi 'Privaldinho’ kupitia mtandao wa instagram na video yao kusambaa kwa kasi.

Katika maongezi yao, Aziz KI alisikika akisema Dube anaenda Yanga ambapo atakuwa kikosini hapo sambamba na Joseph Guede, huku yeye akipambana kuwafanya wawe wafungaji bora msimu ujao.

“Dube anakuja, Guede yupo, nisikilize, mimi ni kiungo, nitafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanakuwa wafungaji bora. Mimi ni kiungo kwa nini niwanie ufungaji bora, kwa nini ununue straika halafu utake kiungo awe mfungaji bora?” Amehoji Aziz Ki na kuongeza.

“Mimi ahadi yangu, nina matumaini straika wa Yanga atakuwa mfungaji bora msimu ujao Mungu akipenda, lakini sio Aziz, sahau kuhusu Aziz, mimi nitatoa asisti na siyo kuwa mfungaji bora.”

Aziz KI aliyejiunga na Yanga misimu miwili iliyopita akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, amefanikiwa kuipa Yanga mataji mawili mfululizo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).

Kiungo huyo ambaye msimu uliomalizika ameibuka kinara wa mabao Ligi Kuu Bara akifunga 21, katika misimu miwili kikosini hapo amecheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (2022-2023) na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (2023-2024).

Hivi karibuni, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, alisema kuelekea msimu ujao watahakikisha wanasajili wachezaji wazuri ambao wanahitajika na benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Miguel Gamondi, huku akisisitiza mchezaji wanayetaka abaki kikosini hapo watahakikisha haondoki.

Aziz Ki baada ya kuonyesha uwezo mkubwa ndani ya Yanga, inaelezwa kwamba amepata ofa nyingi zikiwemo kutoka nchini Afrika Kusini zikihitaji saini yake.