Prime
Aziz KI apewa mambo wawili Yanga
YANGA inarudi uwanjani leo ikiikaribisha JKT Tanzania katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara na kama utamuona kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Stephanie Aziz KI akipewa nafasi ya kucheza, basi inatokana na kazi moja maalum inayoendelea kufanyika kwenye eneo la mazoezi.
Ndani ya mazeozi ya Yanga, kocha wa timu hiyo, Manqoba Mngqithi amefanya uamuzi katika kumboresha kiungo huyo akimpa muda maalum na makocha wawili wanaofanya kazi ya kumpandisha ubora.
Aziz KI ana muda maalum wa kuanza mazoezi akiwa na kocha Chyna Mokaila, ambapo kiungo huyo amekuwa akipewa mazoezi maalum ya kumuongezea utimamu wa mwili akitumia dakika 30.
Baada ya mazoezi hayo, Aziz KI anakutana na kocha wa mipira ya kutengwa, Kagisho Dikgacoi, huku akipewa mazoezi mengine ya ufundi akisimamiwa na mtaalamu huyo wakitumia dakika 15 hadi 20.
Akimaliza hapo, Aziz KI amekuwa akijumuika na wachezaji wengine kwa ujumla akiendelea na mazoezi kamili na kikosi hicho ambapo huko anakutana na mastaa wengine akiendelea kutafutiwa muunganiko na wenzake.
Mbali na Aziz KI, ratiba hiyo pia ilikuwa unamuhusisha mshambuliaji wa timu hiyo, Seleman Mwalimu ambapo wawili hao ndio wachezaji wa mwisho wawili kusajiliwa kwenye kikosi hicho wakikosa sehemu kubwa ya maandalizi ya timu.
Kwenye mazoezi hayo na wenzake, Aziz KI amekuwa akipewa majukumu ya kucheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho kama namba kumi, huku akionyesha ubora wake wa kupiga pasi kwenda kwa washambuliaji.
Akizungumza kuhusu Aziz KI, kocha wa Yanga, Mngqithi, amesema bado kazi ya kumpandisha ubora kiungo huyo inaendelea ambapo akiwa tayari ataanza kuonekana kwenye mechi za timu hiyo.
“Unajua kwamba Aziz KI alichelewa kujiunga na timu, kwahiyo kuna mambo lazima yafanyike ili kuwa sawa na wenzake, wakati ukifika akionekana yupo sawa mtamuona uwanjani,” alisem Mngqithi.
Aziz KI amerejea Yanga msimu huu baada ya kuondoka 2024-2025 akitimkia Wydad ya Morocco ambayo alidumu kwa takribani miezi sita, akajiunga na Al Ittihad ya Libya ambayo nayo alicheza miezi sita, ndipo akatua Yanga.
Kiungo huyo raia wa Burkina Faso, awali alitua Yanga msimu wa 2022-2023 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, katika kipindi cha misimu mitatu akiwa Yanga, aliandika rekodi kadhaa ikiwemo ya kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara 2023-2024 akipachika mabao 21, huku pia msimu huo akiwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu (MVP).
Kurejea kwake Yanga, mashabiki na viongozi wa timu hiyo wana matumaini ataendelea kufanya vizuri kama ilivyokuwa awali, huku hadi sasa kikosi hicho kikiwa kimecheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara, bado hajapata nafasi ya kuonekana uwanjani tangu alipotambulishwa Agosti 15, 2026, siku ambayo dirisha la usajili lilifungwa.