Azam FC, kanyaga twende Misri
Muktasari:
- Mchezo huo utaongozwa na mwamuzi wa kati Simoes Bernardo Guambe kutoka Msumbiji, aliyeteuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
AZAM FC inaanza safari ya kusaka mafanikio katika Kombe la Shirikisho Afrika leo, Ijumaa, itakapokuwa ugenini nchini Misri kuvaana na ZED FC katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya awali ya mashindano hayo.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa saa 2:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, huku Azam ikilenga kupata matokeo mazuri yatakayoipa nafasi nzuri kabla ya mchezo wa marudiano utakaochezwa Oktoba 24, 2026, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema maandalizi ya kikosi chake yamekamilika kwa kiwango kikubwa, huku wachezaji wakiwa na morali nzuri kimwili na kiakili.
“Tumekuwa na takribani siku tatu nzuri za maandalizi kwa ajili ya mechi yetu dhidi ya ZED FC. Itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wetu wanacheza nyumbani, lakini tutaonyesha uwezo wetu kabla ya kurudiana tena jijini Dar es Salaam,” amesema Ibenge.
Kocha huyo raia wa DR Congo alisisitiza kuwa Azam haitawadharau wapinzani wao licha ya kutokuwa na uzoefu mkubwa katika mashindano ya klabu ya Afrika.
Amesema ndiyo sababu kikosi kimewasili kikiwa na wachezaji muhimu, kikilenga kupata matokeo yatakayowapa nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata.
Azam ilianza moja kwa moja raundi ya pili ya awali na sasa inahitaji kutumia vizuri mchezo wa kwanza ili kupunguza presha ya marudiano itakapokuwa mwenyeji Chamazi.
Kwa upande wao, ZED FC ilifuzu raundi hii baada ya kuiondoa ASAS Djibouti Telecom ya Djibouti kwa jumla ya mabao 5-1. Katika mchezo wa kwanza nchini Misri, ZED ilishinda mabao 4-0 kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini.
Klabu hiyo ya Misri, iliyokuwa ikifahamika awali kama FC Masr na yenye makao yake Giza, haina historia ndefu katika mashindano ya kimataifa ya CAF. Msimu huu wa 2026/27 ni mara yake ya kwanza kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Mchezo huo utaongozwa na mwamuzi wa kati Simoes Bernardo Guambe kutoka Msumbiji, aliyeteuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).