Askari zaidi ya 400 waimarisha ulinzi Kariakoo Dabi
Muktasari:
- Zaidi ya askari 400 wa Jeshi la Polisi wapo uwanjani hapo, wakiwemo waliovalia magwanda na wengine waliovaa kiraia, huku wakihakikisha hakuna mtu anayeingia na mabango yasiyohusiana na dabi hiyo.
TOFAUTI na hali inavyoonekana kwa jicho la kawaida, kwamba hakuna hekaheka kubwa katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, kunakosubiriwa kupigwa mechi ya Kariakoo Dabi, Simba ikiwa mwenyeji wa Yanga, kwa upande wa askari kazi si ndogo.
Zaidi ya askari 400 wa Jeshi la Polisi wapo uwanjani hapo, wakiwemo waliovalia magwanda na wengine waliovaa kiraia, huku wakihakikisha hakuna mtu anayeingia na mabango yasiyohusiana na dabi hiyo.
Baada ya Mwanaspoti kuona dabi hiyo haina shamrashamra kubwa na mashabiki hawajitokezi kwa wingi kama ilivyo katika dabi nyingine, ambazo huambatana na foleni za watu wanaoingia uwanjani na uwanja kujaa, lilimfuata ofisa wa ngazi za juu ili kujua majukumu yao yalivyo.
Katika mazungumzo na Mwanaspoti, ofisa wa Jeshi la Polisi Tanzania mwenye cheo cha Mratibu wa Polisi (SP), Mohammed Manyahe, maarufu kama Afande Muddy, amesema leo uwanjani hapo kuna askari zaidi ya 400.
"Majukumu ya askari hayategemei wingi wa watu. Hata kama kuna watu wawili, tutaendelea na majukumu yetu. Hata kama geti limefungwa, kama mechi inachezwa, bado tutafanya majukumu yetu," amesema Manyahe na kuongeza:
"Mechi za Simba na Yanga kwa Tanzania ni za VVIP, tunazipa uzito wake. Ndiyo maana hatuwezi kuruhusu mabango ambayo hayahusiani na mechi, kwa sababu tunataka mchezo uende vizuri."
Aliongeza kuwa majukumu ya askari hayaamuliwi na wingi wa watu, bali hutegemea mpango mkakati uliowekwa.
"Kama wengine wanaona hakuna presha, askari ana jicho lake la kufanya kazi. Katika mechi nyingine, wastani wa askari huwa 300," amesema.
Saa 1:00 usiku itapigwa mechi ya Simba na Yanga katika Uwanja wa Uhuru, ambapo msimu uliopita wa 2025/26, katika mechi ya mzunguko wa kwanza ambayo Wanajangwani walikuwa wenyeji, timu hizo zilitoka suluhu. Katika mechi iliyopigwa Meja Jenerali Isamuhyo, Wekundu wa Msimbazi walitoka sare ya mabao 2-2.