Aloyce Chilongola ataja kinachombeba Fountain Gate
Muktasari:
- Pia amesema ikiwa ni msimu wake wa kwanza kucheza ligi hiyo, malengo yake ni kutumia nafasi hiyo kuonesha kipaji chake ili kujitangaza katika medani za soka ndani na nje.Chilongola amejiunga na Fountain Gate baada ya kupandishwa kutoka timu ya vijana aliyojiunga nayo msimu mmoja kufuatia kufuzu majaribio yaliyofanyika Gairo, Morogoro na sasa anakimbiza Ligi Kuu.
PAMOJA na kuchekelea kiwango chake Ligi Kuu Bara, kiungo mshambuliaji wa Fountain Gate, Aloyce Chilongola amekiri ugumu wa ligi hiyo akieleza kuwa inahitaji nguvu na juhudi binafsi katika kuipa matokeo mazuri timu hiyo.
Pia amesema ikiwa ni msimu wake wa kwanza kucheza ligi hiyo, malengo yake ni kutumia nafasi hiyo kuonesha kipaji chake ili kujitangaza katika medani za soka ndani na nje.Chilongola amejiunga na Fountain Gate baada ya kupandishwa kutoka timu ya vijana aliyojiunga nayo msimu mmoja kufuatia kufuzu majaribio yaliyofanyika Gairo, Morogoro na sasa anakimbiza Ligi Kuu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kinda huyo amesema kiwango alichonacho ni kutokana na ufundi anaopewa na kocha Fred Felix ‘Minziro’ lakini kujituma na kupambania ndoto zake.
Amesema licha ya ubora wake uwanjani na kuaminiwa kupewa nafasi kwa mechi zote, lakini Ligi Kuu ni ngumu akieleza kuwa wapo baadhi ya mastaa wakiwamo Mudathir Yahya na Salum Aboubakari ‘Sure Boy’ anaojifunza kitu kwao.
“Kikubwa ni kupambana na kujituma, kocha ananipa ufundi mwingi lakini hata ile kuniamini kunipa namba inanongezea zaidi makali kufukuzia ndoto zangu, Fountain Gate ni sehemu ya daraja kwangu kufikia malengo.”
Kuhusu matokeo ya jumla ya timu, nyota huyo amekiri hali kutokuwa nzuri, akieleza kuwa mechi sita na kukusanya nne pointi si mwanzo mzuri kutokana na malengo na matarajio yao.
“Lazima tupambanie timu kuhakikisha haishuki daraja, kutokana na malengo yetu bado tunaweza kubadili upepo huu na kuiweka pazuri timu msimamo, uwezo tunao na nia ipo,” amesema kiungo huyo.