AFCON 2027 yawavuta Waarabu Zanzibar
Muktasari:
- Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji mwenza wa AFCON, fainali zitakazofanyika Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027 pamoja na Kenya na Uganda. Amesema, hatua hiyo inakuja kufuatia historia ndefu na undugu wa damu uliopo kati ya Zanzibar na Oman, jambo linalofanya safari hiyo kuwa zaidi ya utalii wa michezo, bali ni fursa ya kutembelea ndugu, jamaa pamoja na kujionea utamaduni wa pamoja.
VIONGOZI mbalimbali kutoka Oman, wamesema wamevutiwa na mazingira ya Zanzibar hivyo watawashawishi wananchi wa nchi hiyo kuja kushuhudia Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027) kisiwani hapa.
Kauli hiyo imetolewa na Abdallah Al-rubaiey katika kongamano la waandishi wa habari wa Zanzibar na Oman lililofanyika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Unguja.
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji mwenza wa AFCON, fainali zitakazofanyika Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027 pamoja na Kenya na Uganda. Amesema, hatua hiyo inakuja kufuatia historia ndefu na undugu wa damu uliopo kati ya Zanzibar na Oman, jambo linalofanya safari hiyo kuwa zaidi ya utalii wa michezo, bali ni fursa ya kutembelea ndugu, jamaa pamoja na kujionea utamaduni wa pamoja.
Abdallah ambaye ni Msimamizi Mkuu wa Kongamano hilo, amesema kufanyika kwa AFCON kisiwani hapa itakuwa fursa kubwa kwa wananchi wa Oman kufika kujionea uzuri wa kisiwa hiki. Amesema, maandalizi makubwa yanayofanywa na Serikali ya Zanzibar, ikiwemo ujenzi wa viwanja vya michezo na miundombinu ya barabara yanakamilisha hamu yao ya kushuhudia mechi za kimataifa katika mazingira ya Zanzibar.
“AFCON 2027 itakuwa fursa nzuri kwetu kuendeleza umoja na mshikamano, hivyo nitawashawishi wananchi wa Oman kufika kisiwani hapa kusherehekea mashindano hayo kudumisha uhusiano wetu wa kihistoria,” amesema.
Kiongozi huyo amesema wanalenga kupata ushawishi na ukuaji kutokana na ujio wa wageni wengi kutoka Oman na duniani kote wakati wa mashindano hayo.
AFCON 2027 kwa upande wa Tanzania, viwanja vitakavyotumika ni Benjamin Mkapa (Dar es Salaam), Samia Suluhu Hassan (Arusha) na Fumba (Zanzibar).