Adolf Mtasingwa mdogo mdogo Kaizer
Muktasari:
- Mtasingwa aliingia kipindi cha pili, hatua inayoendelea kuonyesha Kocha wa Kaizer Chiefs, Fernando Da Cruz anamwingiza taratibu kwenye mfumo wa timu hiyo.
MTANZANIA Adolf Mtasingwa ameendelea kupata nafasi kwenye kikosi cha Kaizer Chiefs baada ya kucheza dakika 23 akitokea benchi katika mechi ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Polokwane City.
Mtasingwa aliingia kipindi cha pili, hatua inayoendelea kuonyesha Kocha wa Kaizer Chiefs, Fernando Da Cruz anamwingiza taratibu kwenye mfumo wa timu hiyo.
Kiungo huyo aliyejiunga na Kaizer msimu huu akitokea Azam FC, alianza kupata nafasi kwenye kikosi cha Amakhosi kwenye mechi dhidi ya Golden Arrows timu hiyo ikipoteza kwa bao 1-0 Mtasingwa akicheza dakika 87.
Mechi iliyofuata ilikuwa dhidi ya Mamelodi Sundown alicheza dakika nane na mechi ya juzi dhidi ya Polokwane alipoingia akitokea benchi.
Sare hiyo imeifanya Kaizer Chiefs kufikisha michezo sita bila kupoteza, ikiwa imeshinda mitatu na kutoka sare tatu. Mwanzo huo unaipa timu hiyo mwendelezo mzuri huku Mtasingwa akitafuta nafasi kubwa zaidi ndani ya kikosi.
Kocha anaonekana kumpa nafasi hatua kwa hatua. Dakika 23 alizocheza dhidi ya Polokwane ni sehemu ya safari hiyo, huku lengo la Mtanzania huyo likiwa ni kutumia kila nafasi anayopata kujenga imani zaidi kwa benchi la ufundi.