Aden Rage amjibu Dalali
Baadhi ya viongozi wa Simba wakijadili jambo, Dalali amechukua fomu za kugombea tena uenyekiti habari kamili soma pembeni.
VICKY KIMARO WAGOMBEA uongozi kwa nafasi mbali mbali ndani ya Simba sasa wamefika 22 huku aliyekuwa Makamu wa Pili wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ismail Aden Rage akifunga mtaa jana Ijumaa mchana baada ya kurudisha fomu kwa mbwembwe huku akisindikizwa na umati mkubwa wa watu. Rage alisindikizwa na msafara lukuki wa magari ikiwa ni kujibu mapigo ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali ambaye pia alifunga mtaa wa Msimbazi yaliko makao makuu ya klabu hiyo, mapema wiki hii wakati akichukua fomu za kutetea kiti chake. Katibu huyo wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT), anajitosa kwa mara nyingine kwenye anga za uongozi wa Simba baada ya kushika wadhifa wa Katibu Mkuu lakini alibwagwa kwenye uchaguzi wa mwaka 1985 na fundi cherehani, Mohamed Kavigha. Mbali na Rage, ambaye aliwahi kuchezea timu hiyo kwenye miaka ya 1970, mjumbe wa zamani wa Kamati ya Utendaji, Charles Hamkah na mwanamama Zuwena Matingwa, ambaye anawani nafasi ya kiti cha wanawake kwenye Kamati ya Utendaji wamechukua fomu. Zuwena anakuwa mwanamke pekee mpaka sasa kujitokeza kuwania uongozi ndani ya klabu hiyo ya mtaa wa Msimbazi na alisindikizwa na kundi la kin a mama. Mpaka sasa kwa upande wa wagombea nafasi ya Mwenyekiti wapo sita ambao ni Dalali, Rage, Mohamed Nyali, Michael Wambura, Andrew Dita Tupa na Zakaria Hans Pope wakati kwa upande wa Makamu wa mwenyekiti ni Mwina Kaduguda na Godfrey Nyange 'Kaburu'. Nafasi ya ujumbe ni Mwandishi Mwandamizi Bonifance Wambura, Said Pamba, Suleiman Zakazaka, Shehe Shauli, Sued Nkwabi, Hamis Sued, Hamis Nkoma, Vitas Lipagile, Said Mohamed Kubenea, Shaban Geva, Yasin Mwete, Hassan Shabaan Mgena, Francis Mbeda na Shaaban Geva. Akizungumza jana Ijumaa Katibu wa kamati ya uchaguzi, Khalid Kamguna alisema leo Jumamosi ndio mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu huku kamati yake ikikaa Aprili 12 kupitia majina ya wagombea wote na Aprili 13 wataweka wazi wagombea waliopitishwa. Alisema Aprili 14 na 15 ni kipindi cha pingamizi na kamati yake itakaa tena Aprili 16 kujadili pingamizi hizo kama zitakuwepo kabla ya kutoa siku tano za rufaa na kuruhusu kuanza mchakato wa kampeni. Uchaguzi wa klabu umepangwa kufanyika Mei 9 kwenye ukumbi wa Bwala la Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.