Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makonda ampa deni Samatta

Muktasari:

Naye Salama Jabir alisema kuwa wachezaji wa Stars wanatambua umuhimu wa mchezo huo hivyo wanapaswa kuungwa mkono.

HAPANA shaka kuwa kamati ya hamasa ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha timu hiyo inaibuka na ushindi dhidi ya Uganda kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa.

Kamati hiyo imekuwa ikifanya juhudi kuhakikisha kunakuwa na hamasa kwa mashabiki na wachezaji wa Stars ili kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo ili iweze kufuzu AFCON lakini itategemea pia Cape Verde iibuka na ushindi au itoke sare na Cape Verde.

Chini ya mwenyekiti wake Paul Makonda, ambaye ni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, kamati hiyo imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha lengo kuu la kuundwa kwake linatimia.

Hamasa ya wadau

Kwa kiasi kikubwa hamasa hiyo imefanikiwa kuhamasisha watu maarufu kuhamasisha Watanzania wajitokeze kwenye Uwanja wa Taifa, Jumapili ili mkakati wa kuifunga Uganda uweze kutimia

Kundi hilo linajumuisha wachambuzi na waandishi mahiri wa soka, waigizaji, wasanii, viongozi wa klabu za soka, wamiliki wa mitandao pamoja na wadau wengine.

“Tuko kwenye kipindi ambacho taifa letu linaanza kupeperusha bendera ya soka ndani na nje ya Afrika. Na namna pekee ya kuonyesha kuwa tupo kwenye muelekeo mzuri wa mpira wa miguu kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Uganda.

Kwa kile ambacho kila mmoja wetu anaona kinaweza kuongeza hamasa ili kuiwezesha timu yetu iweze kuibuka na ushindi kifanywe.Niendelee kuwashukuru watu wote mashuhuri walioamua kuibeba Taifa Stars. Niwashukuru kwa sababu wameacha shughuli zao na kuisapoti Taifa Stars,” alisema Makonda.

Viingilio chini, tiketi bure

Katika kudhihirisha ni kwa jinsi gani kamati ya Makonda imesaidia kuongeza hamasa kuelekea mchezo huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepanga bei ya chini ya kiingilio kwenye mechi hiyo kuwa Sh 2000.

Makonda alisema kuwa ana imani kubwa kuwa kiasi hicho ni rafiki na muitikio utakuwa chanya huku akifichua juhudi binafsi za baadhi ya wadau ambao, wamenunua idadi kubwa ya tiketi ambazo watazigawa bure kwa watu ili waweze kutazama mchezo huo akiwemo yeye mwenyewe.

“Nimeridhika zaidi kwa kamati ya hamasa kuwalipia watu takribani 1,300 waweze kuangalia mechi. Lakini, pia ndugu yetu Joseph Kusaga naye amenunua tiketi 1000, huku pia wasanii wakinunua tiketi 500.

Nimeona niungane na ndugu zangu hawa kwa kununua tiketi 1000 ambazo ni kwa ajili ya vijana waishio katika vituo vya watoto yatima ili nao waweze kuangalia mpira,” alisema Makonda.

Mikakati mingine

Makonda ameainisha mikakati mingine ambayo kamati hiyo chini ya uongozi wake imeipanga ili kuhakikisha umati mkubwa wa Watanzania unajitokeza kutazama mchezo huo na kuisapoti Stars.

“Ndugu zetu wa daladala nimewaomba kokote walipo wasafirishe mashabiki ambao, watakuja uwanjani hata kama watakatiza ruti pasipo bhughudha yoyote.

Na ikitokea wakasumbuliwa, wanipigie simu wataachiwa.

Lakini, kampuni zinazotengeneza vinywaji zimeniomba niwape muda wa saa sita baada ya mchezo ikiwa tutafuzu, wauze vinywaji kwa nusu ya bei, hivyo nimekubaliana na hilo na siku hiyo tutafunga baadhi ya mitaa ili kusherehekea,” alisema Makonda.

Makonda amewasisitiza mashabiki kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwani fursa hiyo ni ya muhimu na ya kipekee.

Maoni ya Wadau

“Huu ni wakati wa kizazi cha sasa kuwa sehemu ya historia. Wengi wetu hatukushuhudia wakati Stars inafuzu fainali hizo mwaka 1980 hivyo ni vyema tukaitumia vyema fursa hii,” alisema mwandishi na mchambuzi wa soka wa Gazeti la Mwanaspoti, Edo Kumwembe.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya alisema huu ni wakati wa kuweka kando itikadi za kitimu.

“Hili jambo ni letu. Tuachane na yale mambo ya kusema timu hii imejaza wachezaji wa klabu fulani au haina wachezaji wa timu fulani na badala yake tuungane pamoja na kuishangilia timu ya taifa,” alisema Kaya.

Mtangazaji maarufu Salama Jabir na muigizaji Jacob Stephen ‘JB’ walisema kuwa uwingi na sapoti kubwa ya mashabiki vina nafasi kubwa ya kuiwezesha Stars kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo.

“Bahati nzuri mimi nilikuwepo wakati Peter Tino anafunga bao lililotuvusha kwenda AFCON mwaka 1980 lakini kuna kundi kubwa halikushuhudia sasa ni wakati wa kutimiza hilo.

Nawaomba ndugu zangu tujitokeze na kuisapoti timu,” alisema JB.

Naye Salama Jabir alisema kuwa wachezaji wa Stars wanatambua umuhimu wa mchezo huo hivyo wanapaswa kuungwa mkono.

“Tunaweza kujiona sisi tunaumia sana lakini kiukweli wao wanaweza kuwa wanaumia zaidi pindi wanapofungwa hivyo tuungane nao na kuwapa sapoti,” alisema Salama.