Nguvu kubwa sasa tuweke kimataifa!
Muktasari:
- Bila shaka dabi hii ni jambo kubwa kwa wapenda soka wa Tanzania, lakini sasa ni wakati wa kugeuza macho na masikio yetu yote kwenye jukumu kubwa zaidi michuano ya kimataifa ya CAF.
DABI ya Kariakoo imepita, hisia za mashabiki zimetulia, na historia mpya imeandikwa. Yanga SC waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba SC, ushindi ambao umeendeleza rekodi ya kutawala watani wao wa jadi mara sita mfululizo.
Bila shaka dabi hii ni jambo kubwa kwa wapenda soka wa Tanzania, lakini sasa ni wakati wa kugeuza macho na masikio yetu yote kwenye jukumu kubwa zaidi michuano ya kimataifa ya CAF.
Kwa muda mrefu tumekuwa tukipima uwezo wa timu zetu kupitia michezo ya ndani. Tumeshuhudia ushindani mkali wa Ligi Kuu Bara, tumefurahia mabao, ufundi na mbwembwe za mashabiki kwenye viwanja vyetu. Hata hivyo, hadhi ya taifa kisoka haitapimwa kwa matokeo ya ndani pekee, bali kwa namna klabu zetu zinavyoweza kusimama imara barani Afrika. Ndiyo maana sasa tunapaswa kuunganisha nguvu kubwa kimataifa.
Kwa upande wa Tanzania Bara, tunabebwa na mabingwa Yanga SC ambao tayari wameshaonyesha ubora wao, Simba SC ambao ni wakongwe kwenye ramani ya Afrika, Azam FC wenye nidhamu ya kisasa ya uendeshaji, na Singida Black Stars ambao wana kiu ya kujidhihirisha kimataifa. Kutoka visiwani Zanzibar, tuna KMKM SC na Mlandege SC, timu ambazo zinawakilisha historia na heshima ya soka la Zanzibar. Hizi ndizo timu sita ambazo kwa sasa ndizo mabalozi wetu wa michezo katika anga ya CAF Champions League na CAF Confederation Cup.
Changamoto kubwa kwa klabu zetu imekuwa ni kushindana na nguvu za kifedha, uzoefu na miundombinu ya klabu kubwa za Afrika Kaskazini na Magharibi. Timu kama Al Ahly, Wydad Casablanca, Esperance au TP Mazembe zimejijengea jina kutokana na uwekezaji mkubwa na mpangilio bora wa kiufundi. Hata hivyo, hiyo isiwe sababu ya kukata tamaa. Yanga na Simba tayari zimeonyesha kwamba wana uwezo wa kushindana nao. Tumeshuhudia Yanga ikitinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, tukashuhudia Simba ikifika hiyo pia msimu uliopita na hatua za robo fainali za Ligi ya Mabingwa mara kadhaa. Hivi ni vielelezo kwamba tunaweza, iwapo tutadumisha mshikamano na kuongeza ubora.
Ni wajibu wa kila mdau wa soka nchini kuona kwamba timu zetu zinapata mazingira bora ya kufanikisha safari hii. Viongozi wa klabu lazima wahakikishe maandalizi mazuri, wachezaji watumie nidhamu na kujituma uwanjani, huku mashabiki wakitoa sapoti ya dhati bila kugawanyika kwa ushabiki wa ndani. Katika hatua hii, ushindi wa Yanga ni ushindi wa Tanzania, matokeo ya Simba ni fahari ya taifa, mafanikio ya Azam, Singida Black Stars, KMKM na Mlandege ni heshima kwa Watanzania wote.
Tunapaswa kuamini kuwa huu ndio wakati wetu. Ikiwa timu zetu zitajifunza kutokana na makosa ya nyuma, zitawekeza kwenye mipango ya muda mrefu na kujiamini, basi heshima ya Tanzania kwenye soka la Afrika itaongezeka.
Nguvu kubwa sasa tuziweke kimataifa. Tuwe pamoja kama taifa, tuache maneno ya kubezana, tuunganishe sauti na nguvu. Kwa pamoja, tunaweza kuona bendera ya Tanzania ikipepea kwenye hatua za juu za michuano ya CAF, na siku moja tutashuhudia kombe kubwa la Afrika likibebwa na timu kutoka nyumbani kwetu. Huo ndio wajibu wetu.