Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuondoka Fadlu Simba iwe funzo

KUONDOKA Pict

Muktasari:

  • Msimu uliopita tulishuhudia Yanga ikipoteza makocha wawili Saed Ramovic na Miloud Hamdi na wote walitimkia kwa vigogo wa Kiarabu.

TATIZO kubwa kwa timu za Tanzania, hasa Simba na Yanga hivi sasa ni kupoteza makocha au wachezaji nyota kutokana na kuvutwa na klabu zenye nguvu kubwa ya kifedha za Afrika Kaskazini. Hali hii si mpya.

Msimu uliopita tulishuhudia Yanga ikipoteza makocha wawili Saed Ramovic na Miloud Hamdi na wote walitimkia kwa vigogo wa Kiarabu.

Wiki hii, Simba imepata pigo baada ya Fadlu Davids kuondoka ghafla na kujiunga na Raja Casablanca, huku timu ikiwa na mechi mbili muhimu ndani ya wiki. Kwa mtazamo hali kama hiyo haina budi kuibua mjadala mpana wa kimkakati.

Ikiwa kweli Simba na Yanga, na kwa upana wake soka la Tanzania, zinataka kupiga hatua katika ramani ya soka la Afrika, basi hazina budi kuwekeza katika mpango mbadala wa ndani utakaowezesha kuwapo kwa uthabiti hata pale makocha na nyota wao wanaponyakuliwa.

Hakuna timu inayoweza kufanikiwa kubeba ubingwa wa Afrika ikiwa haina uthabiti wa kiufundi pale inapokumbwa na misukosuko.

Kwanza, tunapaswa kujiuliza kwa nini klabu za Afrika Kaskazini kila mara ndizo zinazoondoka na makocha na wachezaji wetu bora? Jibu ni moja tu uwezo mkubwa wa kifedha unaoambatana na mipango ya muda mrefu. Timu hizo zimejipanga kuwekeza katika rasilimali watu na mifumo jambo linalozifanya ziwe na mvuto mkubwa.

Hivyo basi, Simba na Yanga zinapaswa kuiga mfumo huo, lakini zikitengeneza ladha ya ndani inayozingatia mazingira yetu. Mojawapo ya mapendekezo ya msingi ni kuwa na benchi pana la ufundi linaloundwa na makocha wenye vigezo vya CAF katika kila ngazi ya timu - kuanzia vijana hadi wakubwa.

Kwa mfano, kama Simba wangeandaa kikosi cha makocha wa vijana wenye ujuzi wa hali ya juu, leo hii kuondoka kwa Fadlu kusingewatikisa.

Kocha wa ndani angetosha kuendeleza falsafa ya timu kwa urahisi. Vilevile, ni muhimu kuwekeza katika wachezaji chipukizi wa ndani.

Kuna nyakati tunashuhudia wachezaji bora wakinyakuliwa na klabu za Misri, Morocco au Algeria. Ili kuzuia pengo hilo, timu zetu zinapaswa kuwa na akiba ya vipaji kutoka akademia zao wenye viwango vya kushindana kimataifa.

Vipaji hivyo vikipewa nafasi na malezi ya kitaalamu, hata wachezaji wakubwa wakiondoka ghafla pengo halitakuwa kubwa.

Ni lazima Simba na Yanga ziwe na msuli wa kimkakati unaozidi presha ya nje na ndani ya uwanja. Mafanikio ya ubingwa wa Afrika hayatapatikana kwa jina kubwa au mashabiki wengi, bali kuwa na majopo ya makocha wenye ubora na uthabiti.

Kuondoka kwa makocha au wachezaji si tatizo jipya, bali ni mtihani wa ukomavu wa kiutawala na uwekezaji wa ndani. Funzo la kuondoka kwa Fadlu, Ramovic na Miloud linapaswa kuziamsha timu zetu ziwe na mpango zaidi ya mmoja.

Ni vyema zisiishi kwa matarajio ya makocha wa kigeni pekee, bali zijenge mfumo wa ndani unaojitegemea. Benchi la ufundi liwe na makocha watatu au wanne wa viwango sawa watakaokuwa tayari kubeba jukumu wakati wowote.

Kwa ujumla, huu ni wakati wa Simba, Yanga na timu nyingine kujipanga kimkakati ndani kwa ndani. Bila mipango thabiti ya ndani tutaendelea kuwa watazamaji wa mafanikio ya wenzetu. Lakini tukijizatiti Tanzania itaandika historia mpya ya soka Afrika hivi karibuni.