Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ishu ya viwanja itaharibu ladha ya Ligi Kuu

VIWANJA Pict

Muktasari:

  • Uamuzi huo ulifikiwa baada ya mchezo wa ufunguzi kati ya wenyeji Tabora United (sasa TRA United) dhidi ya Dodoma Jiji FC, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

JUZI Jumamosi, Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB) ilitangaza rasmi kuufungia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi uliopo mkoani Tabora kwa kushindwa kukidhi vigezo vya kutumika kwenye michezo ya mashindano ya Ligi Kuu.

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya mchezo wa ufunguzi kati ya wenyeji Tabora United (sasa TRA United) dhidi ya Dodoma Jiji FC, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Katika mchezo huo, licha ya matokeo hayo kuwa ya kuvutia kwa wapenda soka, hali ya uwanja iliwakatisha tamaa mashabiki wengi waliotarajia burudani ya kiwango cha juu.

Bodi ya ligi ilieleza wazi uwanja huo haukuwa tayari kwa matumizi, huku hali ya eneo la kuchezea ikiwa mbovu na miundombinu ya jumla kukosa ubora unaohitajika kwa viwango vya Ligi Kuu.

Tukio hili linatoa taswira pana ya changamoto inayolikumba soka la Tanzania, tatizo sugu la viwanja visivyo na ubora. Ni ukweli usiopingika utamu wa ligi huletwa na mchezo mzuri unaoonyeshwa na wachezaji uwanjani na hilo haliwezekani iwapo viwanja ni vibovu.

Viwanja duni huathiri uchezaji, huongeza hatari ya majeraha kwa wachezaji na huwakatisha tamaa mashabiki wanaotoka mbali kufuatilia timu zao.

Mara kadhaa tumeshuhudia baadhi ya timu za Ligi Kuu hulazimika kuhamishia mechi zao viwanja vingine kutokana na viwanja vyao vya nyumbani kushindwa kufikia vigezo. Hali hii huathiri maandalizi ya timu, huondoa faida ya kucheza nyumbani 'home advantage' na huongeza gharama za uendeshaji kwa klabu.

Baada ya msimu wa 2024/25 kumalizika, kulikuwa na kipindi kizuri kwa wamiliki wa viwanja kufanya ukarabati na kuboresha maeneo yote muhimu, hasa sehemu ya kuchezea (pitch), vyumba vya kubadilishia nguo, maeneo ya waandishi wa habari, pamoja na huduma kwa mashabiki. Kwa masikitiko makubwa, baadhi ya viwanja havikufanyiwa marekebisho yoyote licha ya kupewa muda wa kutosha kufanya hivyo.

Kwa msingi huo, tunatoa rai kwa TFF, TPLB na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuweka mkazo mkubwa kwenye ukaguzi wa viwanja kwa wakati. Pia, pawepo na sera au mwongozo wa kitaifa kuhusu matengenezo na usimamizi wa viwanja vya michezo, ili kuhakikisha ubora unadumu msimu mzima na si kwa siku chache tu mwanzoni mwa ligi.

Wakati huo huo, klabu zinapaswa kushirikiana na wadau mbalimbali kama halmashauri, Serikali Kuu na wafadhili kuhakikisha viwanja vyao vinaboreshwa. Ni muhimu pia kuanzisha utaratibu wa mara kwa mara wa kupima ubora wa viwanja wakati ligi inaendelea, ili kuzuia matatizo kabla hayajatokea.

Tunapoukaribisha msimu wa 2025/26 wa Ligi Kuu, tunapaswa kujifunza kutokana na changamoto za awali. Tuweke mbele ustawi wa mchezo wa soka kwa kuwekeza kwenye miundombinu, hasa viwanja. Hatua hii haitasaidia tu timu na mashabiki, bali itachochea maendeleo ya soka la Tanzania kwa ujumla.

Viwanja bora ni msingi wa ligi bora. Bila ya hilo, ladha ya ligi itazidi kufifia. 

Ingawa ni kweli mazingira ya mvua au changamoto za kifedha zinaweza kuchelewesha matengenezo, bado hilo halipaswi kuwa kisingizio cha kushindwa kuhakikisha viwanja vinakuwa katika hali bora kabla ya msimu mpya kuanza.

Ni jukumu la msingi kwa wamiliki wa viwanja, iwe ni Serikali, halmashauri au mashirika binafsi, kuhakikisha viwanja vyao vinatunzwa muda wote. Utunzaji wa viwanja usisubiri wakati wa ligi pekee, bali uwe endelevu kwa misingi ya kitaalamu.

Kufungiwa kwa viwanja kama Ali Hassan Mwinyi kunaharibu ladha ya ligi. Mashabiki ambao wamekuwa na matarajio makubwa ya kuona timu zao zikicheza nyumbani, hujikuta wakikata tamaa na hata kususia mechi.

Hili lina athari kubwa kwa mapato ya vilabu kupitia milango ya viingilio, biashara ndogondogo uwanjani, na hata haki za matangazo ya televisheni. Hakika, uwanja ni zaidi ya sehemu ya kuchezea mpira; ni chanzo cha ajira na mapato kwa jamii inayouzunguka.

Uwanja ukiwa bora huvutia wadhamini, huongeza thamani ya timu na mashindano, na huleta mvuto kwa mashabiki wa ndani na nje ya nchi. Ligi yoyote duniani hupimwa kwa viwango vyake  si tu kupitia wachezaji na timu, bali pia ubora wa viwanja vinavyotumika.